Kwa mujibu wa Shirika la Afya Duniani (WHO) linaloshauri mataifa
kuchukua hatua dhidi ya kisukari, watu milioni 422 wana ugonjwa wa
kisukari kwa sasa na kwamba idadi hiyo inaweza kuongezeka mara mbili
zaidi ndani ya miaka 20 ijayo.
Aidha, imefahamika kwamba watu zaidi ya milioni mbili wanakatwa miguu kutokana na maradhi hayo ya kisukari.
Akizungumza na gazeti hili jana, Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii,
Jinsia, Wazee na Watoto, Ummy Mwalimu amesema ongezeko hilo linatokana
na aina za maisha za watu kwa sasa.
“Kasi ya magonjwa haya inaongezeka kwa kiwango kikubwa sana ingawa
sina takwimu hapa kwa sasa kwa sababu niko mbali, lakini ongezeko ni
kubwa, na hii inatokana na aina ya maisha waliyonayo watu kwa sasa,”
amesema Ummy.
Aliongeza kuwa sababu kubwa ya magonjwa hayo ni ulaji wa watu wa
vyakula visivyokuwa bora na hasa vile vya kusindikwa, kutokufanya
mazoezi na pia kula ovyo.
Alisema serikali kwa sasa imejiwekea mikakati ili kupambana na
magonjwa hayo yasiyoambukiza ambayo ni pamoja na shinikizo la damu,
sukari, saratani na moyo.
“Tulikuwa tunapambana na magonjwa yanayoambukiza kama kipindupindu,
kifua kikuu na mengineyo, lakini sasa na huku kwenye magonjwa
yasiyoambukiza tunaona nako kasi ni kubwa,” alisema.
Aidha, alisema Oktoba mwaka huu, serikali ilianzisha mkakati wa
kitaifa kupambana na magonjwa yasiyoambukiza baada ya kubaini ongezeko
kubwa la magonjwa hayo. Alisema kabla ya kumalizika kwa mwaka huu,
zitazinduliwa kampeni za mkakati huo na Makamu wa Rais, Samia Suluhu
Hassan.
“Kikubwa tutakachofanya ni kutoa elimu ya magonjwa haya, kuhamasisha
ufanyaji wa mazoezi, ulaji sahihi wa vyakula na aina ya vyakula ili
kupunguza tatizo,” aliongeza Ummy. Alisema baada ya uzinduzi yatatolewa
maelekezo katika ngazi zote za uongozi kuanzia ngazi za vijiji nini
wanatakiwa kufanya.
“Kuna watu ambao tutawaingiza katika kampeni hii ambao ni ‘community
workers’ kila kijiji wako wawili, mbali na majukumu yao mengine
watafanya pia kazi ya kutoa elimu hii kwa wananchi, pia tutatumia vyombo
vya habari,” alifafanua zaidi.
Katibu wa Klabu ya Mazoezi Tabata Mawenzi, Said Mgombeni
alithibitisha kuwa ufanyaji wa mazoezi humfanya mtu kuwa mbali na
maradhi mbalimbali na hasa yale yasiyoambukiza kama vile magonjwa ya
moyo na pia kisukari.
“Hapa kwetu tunafanya mazoezi kila siku asubuhi tunakimbia kabla ya
kila mmoja hajaingia katika shughuli zake za utafutaji wa maisha, afya
zetu zinakuwa imara sana tunaamini kwa kufanya mazoezi mtu anakuwa mbali
na magonjwa hayo,” alisema Mgombeni.
Alisema watu wanaweza kujiunga pia na vilabu au vikundi vya mazoezi
ambavyo vimeundwa maeneo mengi ya mijini ili kuweza kuungana nao kufanya
mazoezi bila kupata gharama ya kwenda kwenye mazoezi ya kulipia na
ambapo wanapata pia muda wa kushauriana ulaji sahihi.
Mgombeni aliwashauri watu mbalimbali kujitahidi pamoja na mambo
mengine ya utafutaji wa maisha, lakini pia kupata muda angalau mara
mbili kwa wiki kufanya mazoezi.
Naye Dk Patrick Mirumbe alisema watu wengi na hasa wa mijini wanakula
na kunywa vinywaji vya viwandani kama vile soda na juisi pamoja na
vyakula ambavyo ni hatari kwa maisha yao na hawafanyi mazoezi.
“Watu wanakunywa juisi, soda, vyakula vya kopo ambavyo vinasindikwa
viwandani na bado anatoka nyumbani na gari binafsi, akifika ofisini
anapanda ghorofani kwa lifti na akirudi ni hivyo hivyo na akifika
nyumbani anakaa kwenye televisheni, anakula na kulala, hii ni hatari kwa
afya zao,” alisema Dk Mirumbe.
Amewaasa watu mbali na kufanya mazoezi kujitahidi kula vyakula vya
asili pamoja na juisi za kutengeneza za matunda. Ameshauri pia
kuchunguza afya kila baada ya miezi mitatu.
chanzo;zanzibar24.
Comments