Mama Shein aliyasema hayo leo kwa nyakati tofauti wakati akizungumza
na akinamama, viongozi na wanachama wa Jumuiya ya Wanawake Tanzania
(UWT) wa Wilaya ya Kaskazini A na Wilaya ya Kaskazini B Unguja kwa lengo
la kuwasalimia na kuwashukuru kwa kuendelea kuiunga mkono CCM, na
kupelekea kupata ushindi wa kishindo katika uchaguzi uliopita.
Akiwa katika ukumbi wa Korea, huko Kibokwa Wilaya ya Kaskazini A,
Mama Shein alieleza kuwa kila mtu kwa nafasi yake ailinde amani na
kuinukuu kauli ya Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi
Dk. Ali Mohamed Shein anayoitoa mara kwa mara isemayo “hakuna mbadala wa
amani”.
Alisema kuwa mara nyingi kinamama na watoto huwa ndiyo wanaoathirika zaidi wakati amani inapotoweka.
Mama Shein ambaye katika ziara yake hiyo amefuatana na viongozi mbali
mbali wakiwemo wake wa Wabunge na Wawakilishi wa Zanzibar, alisema kuwa
tayari Serikali iliyochaguliwa na wananchi yenye nia ya kweli ya
kuwaletea maendeleo wananchi wa Zanzibar, imeshaundwa na inaendelea na
kazi ya kuwatumikia wananchi kwa ufanisi mkubwa.
Alieleza kuwa Serikali chini ya uongozi wa Dk. Shein inafanyakazi kwa
umakini mkubwa kwa lengo la kutimiza matumaini na matarajio waliyonayo
wananchi wakati walipoichagua.
Hivyo, Mama Shein alisema kuwa ni wajibu wa viongozi na wananchi wote
kutoa ushirikiano katika kuhakikisha kwamba malengo ya Serikali katika
kuinua uchumi na kuimarisha huduma za jamii yanafanikiwa.
Mapema Mama Asha Balozi, Mke wa Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar
alieleza haja ya wanawake kuendelea kupendana huku akisisitiza suala
zima la uadilifu katika mchakato mzima wa uchaguzi ujao wa Chama hicho
hapo mwakani.
Aliwataka akinamama kujipunguzia majukumu na badala yake wawe na
utaratibu wa kujua nyendo za watoto wao hasa kutokana na kukithuri
vitendo vya ubakaji ambavyo vimeendelea kushika kasi katika Mkoa huo.
Nae Mama Fatma Karume kwa upande wake aliwataka akina mama
kuwaelimisha na kuwafunza watoto wao pamoja na kuwasaidia waume zao
katika harakati zote za kisiasa na kimaendeleo.
Alieleza furaha yake kwa kona wanawake waliowengi hivi sasa wamepata
uongozi na wamo madarani jambo ambalo ilikuwa nadra kabla ya Mapnduzi ya
Januari 12, 1964 na kuwataka waliopana fursa hiyo kuitumia vyema na
kuishi na watu vizuri.
Katika risala yao wanachama wa Jumuiya ya UWT walieleza kufarajika
kwao na ujio wa Mama Shein katika Wilaya yao ya Kaskazini A na
kumuhakikishia kuwa wataendelea kuiunga mkono CCM ili iendelee kushika
hatamu.
Akiwa katika ukumbi wa Hoteli ya Sea Cliff huko Kama, Wilaya ya
Kaskazini B, Unguja Mama Shein alitoa wito kwa jamii kuchukua juhudi za
makusudi katika kuhifadhi mazingira na kuielimisha jamii juu ya utunzaji
wa mazingira hayo.
Alisema kuwa maeneo ambayo kwa miaka mingi yamekuwa yakitegemewa kuwa
na vianzio vikubwa vya maji, yameathiriwa kutokana na ukataji wa miti,
na ujenzi wa nyumba bila ya kuzingatia mipango mizuri sambamba na
shughuli za uchimbaji wa mchanga na udongo ambazo zimeathiri sana ndani
ya Mikoa hapa nchini.
Pia, Mama Shein ambaye alipata mapokezi makubwa katika mkoa huo,
alisisitiza suala zima la kushirikiana na Serikali katika kupambana na
ukatili na udhalilishaji wa wanawake na watoto kwani katika jamii
kumeendelea kusikika vitendo vya aina hiyo ambavyo ni aibu, na ni
kinyume cha maadili na mafundisho ya Dini.
Nae Mama Fatma Karume aliwataka akinamama wa Jumuiya hiyo kutojali
maneno na kasumba mbali mbali zinazosambazwa na wapinzani ambazo hazina
manufaa wala nafasi kwa CCM.
Nae Mama Asha Balozi aliendelea kutoa wito kwa wananchi wa Mkoa huo
kupiga vita suala zima la udhalilishaji wa wanawake na kusisitisha
mashirikiano ndani ya Jumuiya ya UWT.
Nao wanajumuiya ya UWT Wilaya ya Kaskazini B, walieleza kuwa haja ya
kuongezewa mitaji na mikopo katika vikundi vyao ili kipato wanachokipata
kiweze kukidhi haja ya malengo yao.
Wakieleza suala zima la udhalilishaji wa wanawake na watoto na
kueleza kuwa suala zima la mashirikiano katika kesi za ubakaji sambamba
na changamoto zilizopo katika mtiririko mzima wa hukumu za kesi za aina
hiyo.
Rajab Mkasaba, Ikulu Zanzibar
chanzo; zanzibar24.
Comments