Mama Shein aliyasema hayo leo kwa nyakati tofauti wakati akizungumza
na akinamama, viongozi na wanachama wa Jumuiya ya Wanawake Tanzania
(UWT) wa Wilaya ya Kusini na Wilaya ya Kati Unguja katika ziara yake
yenye lengo la kuwasalimia na kuwashukuru kwa kuendelea kuiunga mkono
CCM, na kupelekea kupata ushindi wa kishindo katika uchaguzi uliopita.
Akiwa katika ukumbi wa Hoteli ya Karafuu, Michamvi Mkoa wa Kusini
Unguja, Mama Shein alitoa nasaha zake kwa viongozi wa Mkoa na Wilaya
pamoja na wananchi wa Mkoa huo kushirikiana katika kuihami misitu na
miti ya asili ambayo ni muhimu katika kuyahifazi mazingira ambayo ni
hazina kwa vizazi vilivyopo na vijavyo.
Mama Shein, ambaye katika ziara yake hiyo amefuatana na viongozi
mbali mbali wakiwemo Wabunge na Wawakilishi wa Viti Maalum pamoja na
wake wa viongozi wakiwemo Wabunge na Wawakilishi, alitumia fursa hiyo
kusisitiza suala zima la amani na kueleza kuwa bila ya amani hakuna
watakaokwenda kondeni, watakaojishughulisha na kilimo cha mwani, uvuvi
wala utalii na kueleza kuwa watakaoathirika zaidi ni akinamama na
watoto.
Hivyo, aliwataka viongozi na wananchi wa Mkoa huo wasichoke
kuwakumbusha vijana wao umuhimu wa kuitunza amani na kujiepusha na
vitendo vyote vya uvunjaji wa sheria na kuhatarisha amani kwani kuvunja
amani ni mara moja lakini kuirudisha huchukua muda.
Mapema Mama Asha Balozi, Mke wa Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar
aliwaeleza akinamama hao wa Jumuiya hiyo kuwachagua viongozi wenye
uchungu na chama, nchi na wanachama wenzao katika uchaguzi wa Chama na
Jumuiya zake hapo mwakani.
Mama Asha alitumia fursa hiyo kuwataka akinamama wenzake kuwa karibu
na watoto wao ili kuepuka vitendo viovu wanavyoweza kufanyiwa hasa
vitendo vya ubakaji.
Nae Mama Fatma Karume aliwahamisisha wanawake kuchukua fomu za
kugombania nafasi mbali mbali za uongozi ndani ya chama cha CCM bila ya
kuogopa pingamizi za kutowapa nafasi waliokuwa hawakusoma na kueleza
kuwa wengi wao waliofanya Mapinduzi na kuipa uhuru Zanzibar walikuwa
hawana elimu hivyo hicho sio kisingizio.
Alieleza kusikitishwa na vijana ambao hupewa madaraka makubwa ndani
ya serikali na kusahau wajibu na majukumu yao na badala yake kufanya
hilba kwa lengo la kujineemesha wao wenyewe na pale wanapoondoka
madarakani hukimbilia katika vyama vya upinzani.
Aliwaomba wale wote walioteuliwa na Dk. Shein kushika nyadhifa mbali
mbali za uongozi kutomuangusha hasa wanawake ambao katika uongozi wake
amewapa nafasi nyingi serikalini.
Katika risala yao wanachama wa Jumuiya ya UWT Wilaya ya Kusini Unguja
, walitoa shukurani kwa Serikali kwa kuwapelekea mradi wa JOCDO kwa
madhumuni ya kusaidia vikundi mbali mbali ili wajikwamue na hali ngumu
ya maisha ambapo pia, UWT Wilaya imeanzisha vikundi vya Jumuiya katika
Matawi kwa lengo hilo la kujikwamua kimaisha.
Aidha, walieleza kutokuwa nyuma katika kukiimarisha chama na kuleta
maendeleo endelevu na kueleza juhudi walizozichukua katika kuhakikisha
CCM inapata ushindi na kumuahidi Mama Shein kuwa katika Wilaya yao
upinzani hautokuwa na nafasi milele.
Walieleza kusikitishwa na suala zima la unyanyasaji wanawake na
watoto huku wakitumia fursa hiyo kumpongeza Dk. Shein kwa kuendelea
kutekeleza Ilani ya Uchaguzi ya CCM.
Wakati huo huo, akiwa katika ukumbi wa Kituo cha
Elimu kiliopo Dunga, Wilaya ya Kati Unguja, Mama Shein aliwahimiza
akinamama na vijana umuhimu wa kuanzisha na kuviendeleza vikundi vya
maendeleo ili kujiimarisha kiuchumi.
Mama Shein aliwaahidi akinamama hao kuwa wake wa viongozi pamoja na
waheshimiwa wabunge na wawakilisgi wataendelea kushirikiana na vikundi
vya akinamama na vijana katika jitihada zao za kujiletea maendeleo.
Aidha, Mama Shein aliwataka wanajumuiya ya UWT kujitahidi kuzitumia
vyema fursa ambazo Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, Awamu ya Saba
inazitoa kwao kwa lengo la kuwawezesha kiuchumi.
Nao wanajumuiya ya UWT Wilaya ya Kati waliahidi kuendelea kumuunga
mkono Mama Shein katika juhudi zake hizo sambamba na kuendelea kukiunga
mkono chama cha Mapinduzi ili kiendelee kushika hatamu.
Rajab Mkasaba, Ikulu Zanzibar
chanzo; zanzibar24.
Comments