Makamba: Kuzishughulikia kero za Muungano ndio kipaumbele chetu.

makamba1WAZIRI wa Nchi afisi ya Makamu wa rais Muungano Mhe: Januari Yussuf Makamba, amesema kipaumbele cha kwanza ndani ya wizara anayoiongoza, ni kuzishughulikia kero zote Muungano wa Tanganyika Zanzibar, ili kuwe na usawa kwenye utendaji wa kazi kwa pande zote.

Alisema anayodhamira ya kweli ya kuondoa kero, changamoto na malalamiko yanahusua Muungano huo, akiamini kuwa kama hilo litafanyika, linaweza kuimarisha maisha ya wananchi wa pande zote.

Waziri Makamba ameeleza hayo, ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Kaskazini Pemba, mara baada ya kupokea taarifa ya kazi ya mkoa huo, kwenye ziara yake fupi ya kuangalia jengo la Ikulu la Makamu wa rais wa Jamahuri ya Muungano wa Tanzania yalililopo mjini Wete.

Alisema kufanya hivyo, ndio malengo na dhamira za serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar na ile ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, katika kuweka sawa kero za Muungano.

Aidha Waziri huyo alisema, ndio maana wanaangalia uwezekano mkubwa wa kulifanyia matengenezo makubwa jengo la Ikulu kwa ajili viongozi wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, ili wanapofika kisiwani Pemba wawe na makaazi ya uhakika.

“Mimi nisema umoja wetu huu uliopo baina ya serikali zetu mbili, utaimarika zaidi ikiwa kero na malalamiko ya Muungano kwa pande zote zitatuliwa’’,alifafanua.

Waziri huyo alisema jambo lililofanywa na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, kukabidhi jengo hilo kwa Serikali ya Jamhuri ya Muungano, ni faraja na sasa wanajipanga ili kuliimarisha.
Alisema katika ziara yake hiyo, amefuatana na timu ya wataalamu kadhaa wakiwemo wakala wa majengo, ili kufanya tathimini na kuwa na gharama halisi, ili kuangalia bajeti ijayo kama wataweza kuingiza fedha.

Kuhusu uwepo wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, baada ya uchaguzi wa marudio, Waziri Makamba, alisema ipo kihalali na kisheria na wala hakuna mwenye ubavu wa kuiondoa.
Alisema Dk Shein, ni rais halali kwa mujibu wa Katiba ya Zanzibar ya mwaka 1984, na ataendelea kuhudumu akiwa rais wa Zanzibar, hadi uchaguzi mwengine.

Mapema Waziri huyo amewapongeza wafanyakazi wa jengo hilo, kwa kuendelea kulitunza ndani na nje, na kuwaahidi kuwa serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, italifanyia matengenezo makubwa.

Akisoma taarifa ya kazi ya Mkoa wa kaskazini Pemba, Katibu tawala wa mkoa huo Yussuf Mohamed Ali, alisema pamoja na changamoto kadhaa zilizopo, lakini huduma ya maji safi na salama, inapatikana kwa asilimia 88 na hasa baada ya kukamilika kwa mradi wa maji mjini na vijijini.

Aidha, alimueleza Waziri huyo kuwa tatizo la miundombinu ya barabara, yamekaa sawa, hasa baada ya kukamilika kwa barabara tano, zenye urefu wa kilomita 35, zilizojengwa kwa ufadhili wa Mfuko wa Changamoto ya Milenia wa Marekani (MCC).

Mara baada ya kufanya kikao hicho cha kupokea taarifa ya kazi ya Mkoa wa kaskazini Pemba, Waziri Makamba na ujumbe wake, ulilitembelea jengo hilo la Ikulu kwa ajili ya viongozi wa Jamhuri ya muungano wa Tanzania mjini Wete.

chanzo;zanzibar24.

Comments