VIJANA Saba kutoka vyuo vikuu mbalimbali mkoani Dodoma ambao ni
wanachama wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), wameibwaga
serikali katika kesi Na. 127 ya mwaka 2016 iliyokuwa ikiwakabili,
Vijana
hao walikuwa wakikabiliwa na tuhuma za kufanya maandamao bila kibali,
kinyume na Kifungu cha 43 (4) 45, 46 (1) cha Sheria ya Jeshi la Polisi
ambapo Godfrey Pius, Hakimu Mkuu wa Wilaya ya Dodoma ametupilia mbali
kesi hiyo kutokana na serikali kushindwa kutoa ushahidi usiotiliwa
shaka.
Awali ilidaiwa kuwa, tarehe 18 Juni, mwaka huu katika Barabara ya
wajenzi, Area D mjini Dodoma vijana hao waliandamana bila kuwa na kibali
huku wakijua kitendo hicho ni kinyume na sheria.
Waliokuwa wakishitakiwa kwa kesi hiyo ni Pasco Mbele, Andrew Komba, Anna
Joseph, Joseph Buretha, Andrew Mwambene, Lukile Stanslaus na Rosse
Mruchu.
Akisoma hukumu ya kesi hiyo, Hakimu Pius amesema amepitia ushahidi wa
serikali na kubaini kuwa walalamikaji wameshindwa kuithibitishia,
mahakama pasipo kuacha shaka kuwa kulikuwa na maandamano yaliyofanyika
na hivyo kuwaona vijana hao kuwa hawana hatia na kuwaaachia huru.
Amesema kuwa upande wa mashitaka ulipeleka mashahidi wanne ambao wote
walieleza kuwa wanafunzi walikuwa ndani ukumbi wa hoteli ya African
Dream walipokutana kwa lengo la kufanya mahafali ya Chaso na kwamba
Polisi ndio walioenda kuwaondoa katika ukumbi bila kusema sababu za
kufanya hivyo.
Pia imeelezwa kuwa menejimenti ya hoteli hiyo haikuwa imelalamika juu ya
kuwepo uvinjifu wa amani katika eneo hilo kwahiyo hakukuwa na haja ya
Polisi kufika na kusambaratisha kusanyiko hilo.
Hakimu Pius ameongeza kuwa upande wa mashaidi wa serikali, waliulizwa
kama kuna mtu ambaye alifanyiwa fujo au kama waliwaelekeza wanafunzi hao
njia ya kupita baada ya kuwafukuza katika eneo hilo lakini walikiri
kuwa hakuna mtu aliyefanyiwa fujo wala polisi hawakuwaelekeza njia ya
kupita.
Hakimu huyo ameelez kuwa amri y kuwatawanya wanafunzi hao kutoka katika
hoteli husika haikuwa na mashiko yoyote na kwamba wanafunzi hao walikuwa
wana haki ya kukusanyika katika eneo hilo kwa madhumuni husika bila
kubughudhiwa na hoja kuwa waliondoka kwa mandamano haina mashiko pia.
Katika shauri hilo, serikali ilikuwa ikiwakilisha na mwendesha mashitaka
Morice Sarara huku upande wa wanafunzi hao ukiwakilishwa na wakili wa
kijitegemea Elias Machibya.
Itakumbukwa kuwa Jeshi la Polisi Mkoa wa Dodoma lilisambaratisha
mahafali yaliyokuwa yameandaliwa na Umoja wa Wanafunzi wa vyuo vikuu
ambao ni wanachama wa Chadema (Chaso), ambayo mgeni rasmi alikuwa Waziri
Mkuu Mstaafu, Frederick Sumaye huku vijana waliokuwa wakitawanyika
wakikamatwa kwa tuhuma za kuandamana bila kibali.
chanzo;muungwana.co.tz
Comments