Mvua yaezua nyumba 10 Tarime.

MVUA zinazoendelea kunyesha zikiambatana na upepo mkali wilayani Tarime mkoani Mara, zimeleta madhara makubwa katika kata za Sirari, Gwitiryo na Pemba katika Tarafa ya Inchugu kwa kuezua zaidi ya nyumba 10.
Mvua zilizonyesha mwishoni mwa wiki zikiambatana na mawe zilisababisha nyumba moja iliyokuwa na watu ndani, kuangukiwa na bango la Kampuni ya Simu ya Vodacom na kuharibu nyumba hiyo na mali za wakazi hao.
Akizungumza na gazeti hili Ijumaa, Mwenyekiti wa Mtaa wa Sokoni, Benson Makanya alisema mvua hizo zimeleta madhara makubwa katika mji wa Sirari na vitongoji vyake.
“Hapa mnaona nyumba hii ya Mrimi Sagara imeangukiwa na bango hili la Vodacom na kuibomoa vyumba viwili, mali za hawa wapangaji zimeharibika zikiwemo vitanda, ndoo za maji, viti, meza ambapo na maji yamejaa ndani hawana mahala pa kulala. Kwa sasa tunaomba kampuni hii iliyoweka bango hili iweze kufika mapema na kuwajengea nyumba wahanga hawa,” alisema Makanya.
Baadhi ya waathirika wa mvua hiyo ni Amos Marwa, mwenye mke na watoto watano, Mwajuma Raphael, mwenye watoto watatu na Jackson Obando.
“Tulikuwa ndani ya nyumba hii tunayoishi kulitokea mvua kubwa iliyokuwa inaambatana na upepo mkali uliokuwa ukivuma kutokea Kenya, ulipiga bango ambalo liliangukia nyumba tukiwa ndani na kubomoa vyumba viwili na kuharibu samani za ndani vikiwemo vitanda, meza, sahani za udongo, ndoo za maji, chupa za chai na viti,” alisema Marwa.
Mwenyekiti wa Kijiji cha Sokoni Sirari, aliwataja maeneo mengine yaliyoathirika ni ukumbi wa Mohabe Mongo kwa jina maarufu Mwanjelwa, vibanda ya Soko Kuu Sirari na nyumba kumu za kitongoji cha Nyamorege ambazo zimezuliwa. Mazao yaliyoharibiwa na mvua hiyo ya mawe, ni mahindi, maharagwe na migomba kuanguka. Aliiomba serikali kuwasaidia waathirika hao.
chanzo;habarileo.

Comments