Makamo wa Rais wa Shirika hilo la Kimataifa la Maendeleo la Japan
(JICA), Yasushi Kanzaki aliyasema hayo leo huko Ikulu mjini Zanzibar
wakati alipofanya mazungumzo na Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa
Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein.
Katika maelezo yake, Makamo huyo wa Rais wa (JICA) ambaye aliongozana
na uongozi wa Wizara ya Kilimo, Maliasili, Mifugo na Uvuvi, alimueleza
Dk. Shein kuwa Shirika hilo liko tayari kuanza ujenzi huo mapema mwakani
na hivi sasa limo katika hatua za mwisho za matayarisho.
Makamo huyo alisema kuwa mradi wa ujenzi wa soko hilo utakuwa ni wa
kisasa na wa kuvutia kutokana na kukidhi mahitaji yote yanayopaswa
kuwepo kwa ajili ya diko na soko la samaki la kisasa.
Alisema kuwa soko hilo litakuwa la pekee katika ukanda wa nchi za
Kusini mwa Jangwa la Sahara ambapo ujenzi wake unatarajiwa kufanyika
ndani ya muda wa miaka miwili kuanzia muda utakaoanza ujenzi huo.
Aidha, Bwana Yasushi Kanzaki aliahidi kuendelea kuiunga mkono
Zanzibar katika kuendeleza miradi mengine muhimu ya maendeleo ukiwemo
mradi wa kilimo cha mpunga wa umwagiliaji maji, uvuvi na kuendeleza
mradi wa usambazaji maji kupitia Mamlaka ya Maji Zanzibar (ZAWA).
Katika mazungumzo yake kiongozi huyo, alieleza juhudi zinazoendelea
kuchukuliwa na Shirika hilo katika kuimarisha mradi wa maji utakaokwenda
sambamba na teknolojia mpya ya kisasa ili kurahisisha usambazaji na
upatikanaji wa maji safi na salama hapa nchini.
Sambamba na hayo, Makamu huyo wa Rais wa Shirika la (JICA),
alimueleza Dk. Shein matayarisho yanayoendelezwa na Shirika lake na
hatua zilizofikiwa katika kuimarisha mradi wa kilimo cha mpunga wa
umwagiliaji maji kwa mabonde maalum yaliotengwa hapa Zanzibar.
Nae, Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali
Mohamed Shein alitoa pongezi na shukurani kwa Serikali ya Japan kupitia
shirika lake la (JICA) na kueleza kuwa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar
pamoja na wananchi wake wanathamini sana misaada na ushirikiano na
uhusiano uliopo kati yake na (JICA).
Alisema kuwa Shirika la Maendeleo la Kimataifa la Japan (JICA) ni
mshirika muhimu wa maendeleo hapa Zanzibar kwani limeweza kuunga mkono
juhudi za Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar katika kuimarisha miradi
mbali mbali ya maendeleo ikiwemo ya kilimo, maji, afya, elimu, uvuvi na
mengineyo.
Dk. Shein alitumia fursa hiyo kupongeza azma ya ujenzi wa soko hilo
ambapo alisema kuwa utasaidia kuendeleza malengo ya serikali katika
kuimarisha sekta ya uvuvi na kusisitiza kuwa tayari miundombinu ya eneo
linalotarajiwa kujengwa soko ikiwemo umeme na maji lipo katika hatua za
mwisho za matayarisho pamoja na kueleza kuwa tayari ruhusa kutoka UNESCO
nayo imeshatolewa.
Dk. Shein alisema kuwa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar imeweka
lengo la kuanzisha programu ya uvuvi wa bahari kuu ambayo pia,
itawasaidia wavuvi kuvua katika kina kirefu cha maji ili kuongeza
kiwango cha samaki wanaovuliwa na kuongeza fursa za ajira, biashara na
kuchangia ukuaji wa uchumi.
Kwa upande wa kilimo cha mpunga wa umwagiliaji maji, Dk. Shein
alisema kuwa tayari Serikali imo katika juhudi za kuweka miundombinu kwa
kuimarisha eneo la hekta 2,200 katika mabonde ya mpunga huku akieleza
huku akilipongeza Shirika la JICA kwa kuuunga mkono mradi huo.
Alisema kuwa lengo la Serikali katika kuimarisha kilimo hicho ni
kupunguza ama kuondosha kabisa uagiziaji wa mchele kutoka nje ya nchi
unaofanyika hivi sasa kwani matumizi ya mchele hapa nchini ni tani 80
elfu kwa mwaka ambapo kati ya hizo tani 64 elfu huagizwa na
zinazozalishwa nchini ni tani elfu 16 tu.
Dk. Shein alitumia fursa hiyo kutoa pongezi kwa Shirika hilo kwa
kuendelea kuiunga mkono Zanzibar katika kuendeleza mradi wa maji safi na
salama, kwa awamu zote huku akieleza hatua inayofuata ya kuimarisha
mradi huo kwa utaalamu zaidi utasaidia upatikanaji wa huduma hiyo kwa
ufanisi zaidi.
Madhumuni makubwa ya mradi wa ujenzi wa diko na soko la kisasa huko
Malindi ni kuwawezesha wavuvi wanaotumia soko hilo kuuza na kununua
samaki wao wakiwa salama kiafya pamoja na kuwepo mazingira mazuri ya
kuweka vyombo vya uvuvi na biashara kwa wavuvu, wachuuzi, madalali,
wauzaji wadodgo wadogo na wanunuzi.
Tsh. Bilioni 14 zinatarajiwa kutumika katika ujenzi wa soko hilo
ambalo litakuwa na maeneo sita ya kuendesha mnada, meza ndogo 141 za
wauzaji wadogo wadogo, sehemu 13 za kuchakatia samaki, linatarajiwa kwa
siku litakuwa kuegesha vyombo vya uvuvi wa kienyeji 392 na wafanyakazi
1,400 watakaoshusha na kupakia samaki ambapo pia, wafanyabiashara 6,500
watatumia eneo hilo salama.
chanzo; zanzibar24
Comments