SIKU moja baada ya Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania (BoT), Profesa
Benno Ndulu atoe taarifa ya hali ya uchumi nchini inayoonesha uchumi
unakua na deni la taifa ni stahimilivu, wataalamu wa uchumi wamesema,
taarifa hiyo ni sahihi na imetolewa kwa wakati muafaka.
Aidha, wamesema ni vyema wananchi wakaishi maisha ya kipato chao cha
halali, kwani wengi wao walizoea maisha ya juu kutokana na uwepo wa
fedha chafu kwenye mzunguko na sasa mianya hiyo imefungwa ndio maana
fedha zimepungua kwenye mzunguko.
Wakizungumzia taarifa hiyo jana jijini Dar es Salaam, wataalamu wa
uchumi kutoka Chuo Kikuu cha Dar es Salaam(UDSM), walisema ni vyema
wananchi wakaongeza bidii kufanya kazi na kwamba viashiria vyote vya
ukuaji wa uchumi vilivyotolewa na Profesa Ndulu viko sahihi.
“Sina kipingamizi, viashiria vyote vinavyotumika kupima hali ya
uchumi wa taifa viko chanya, hii ni dalili nzuri ni vyema Watanzania
wakakubali kuishi maisha ya uwezo wao, baada ya muda kidogo watazoea,
zile fedha za dili hazipo tena kwenye mzunguko,” alisema Profesa Rozack
Lokina wa Idara ya Uchumi chuoni hapo.
Profesa Lokina akifafanua alisema wananchi wanachotakiwa sasa ni
kufanya kazi kwa tija na kuukubali ukweli kwamba fedha za bure katika
Serikali ya Awamu hii ya Tano hazipo, na kuwataka watu wanaosema uchumi
umedorora, wakaacha kauli hiyo kwa sababu uchumi unapimwa kwa viashiria.
“Mi sioni uchumi ukidorora, watu wanaosema uchumi wa nchi umedorora,
wamepima kwa viashiria gani? Chombo chenye mamlaka ya kutoa taarifa za
uchumi kimetoa taarifa na ndio tunayopaswa kuiamini,” alisema Profesa
Lokina.
Profesa Benson Bana ambaye ni Mhadhiri Mwandamizi wa Udsm alisema,
taarifa hiyo ya BoT imetolewa kwa muda muafaka kwani siku chache
zilizopita watu wenye nia mbaya walieneza taarifa potofu kuwa uchumi wa
nchi umedorora.
“Chombo chenye mamlaka ya kutoa taarifa za hali ya uchumi nchini ni
BoT na Gavana Ndulu amelizungumzia vizuri kwa kutumia viashiria
vinavyotumika duniani, na vimeonesha uchumi wetu unakua kiwango cha
kuridhisha,” alisema Profesa Bana.
Akifafanua hali ya uchumi, alisema suala hilo halihitaji siasa kwa
sababu linatumia viashiria vinavyotambulika kimataifa na ndivyo
vilivyotumika kujua hali ya uchumi ulivyo kwa sasa, ambapo takwimu
zimetolewa Pato la Taifa katika kipindi cha robo ya kwanza ya mwaka
2016, unakadiriwa kuongezeka kwa asilimia 5.5 ikilinganishwa na kipindi
hicho mwaka jana cha asilimia 5.7.
Profesa Bana alisema kuna tofauti ndogo ya asilimia 0.2 ambayo haina
athari yoyote kiuchumi na kwamba tofauti hiyo ni jambo la kawaida na
kwamba mzunguko wa fedha chafu uliokuwepo nchini mianya yake imezibwa,
ndio maana watu wanalalamika hakuna fedha mtaani.
“Unajua fedha chafu ziliingia kwenye mzunguko wa uchumi na sasa
mianya yake imezibwa ni lazima watu walalamike ila cha msingi ni wao
warudi kwenye maisha halisi na wafanye kazi,” alisema Profesa Bana.
Akizungumzia hali ya uchumi wa nchi na mtazamo wake duniani, Profesa
Bana alisema Tanzania inafanya vizuri na kimataifa imekuwa miongoni mwa
nchi 10 barani Afrika ambazo uchumi wake unakua vizuri. Aidha, katika
kiwango cha ukuaji kwa nchi za Afrika Mashariki, Tanzania ni nchi ya
kwanza ambayo uchumi wake unakua vizuri, hivyo kauli za baadhi ya
wanasiasa kujaribu kuupotosha umma kwamba uchumi wa nchi umedorora, sio
jambo sahihi.
“Hapa Gavana alituelimisha kwa njia sahihi na ndiye mwenye mamlaka ya
kutoa takwimu za hali ya uchumi na vigezo vya kimataifa vimetumika sasa
wanasiasa wasijaribu kutafuta umaarufu kwa kusema uchumi umedorora,
uchumi una vigezo vyake,” alisema Profesa Bana.
Alisema jambo la msingi sasa ni kuona ukuaji huo wa uchumi ukimgusa
mwananchi mmoja mmoja na hiyo inawekezana kwa serikali kuhimiza sera
nzuri zitakazosaidia watu kupata fedha kwa kufanya kazi. Naye Dk John
Mtui ambaye ni mtaalamu wa uchumi kutoka Udsm alisema ni vigumu kusema
uchumi wa nchi ni mbaya ingawa fedha kwenye mzunguko zimepungua.
“Hapa kinachoangaliwa ni viashiria vya uchumi, ingawa fedha
zimepungua kwenye mzunguko, hii haimaanishi kwamba hali ya uchumi ni
mbaya, kinachotakiwa ni watu kufanya kazi na kuachana na hulka ya
kungoja fedha za dili,” alisema Dk Mtui.
Alisema watu wakifanya kazi, itawalipa na kwamba fedha chafu
ziliingia kwenye mzunguko kwa wingi kwani wapo baadhi walikuwa wakifanya
biashara bila kulipa kodi, wapo waliokuwa wakipata zabuni kwa njia
haramu na mianya hiyo imezibwa hivi sasa.
“Yaani mambo mengi yaliendeshwa kwa kupeana dili, unakuta mtu ana
kampuni ya kuuza chakula, wanapeana rushwa halafu ile zabuni inaongezwa
fedha ambazo sio halali, zinaingia kwenye mzunguko sasa hayo mambo
yamezibwa watu lazima walalamike,ila hali itatulia baada ya muda“,
alisema Dk Mtui.
Wakati wasomi wakisisitiza hali ya uchumi inaridhisha kutokana na
viashiria vya uchumi, Chama cha Wananchi (CUF), wamemuomba Gavana Ndulu
kuondoa kilio cha ukosefu wa fedha kwa wananchi.
Kwa mujibu wa taarifa ya chama hicho iliyotolewa jana na Naibu
Mkurugenzi Habari, Uenezi na Mahusiano na Umma, Mbarara Maharagande,
ilisema kiuhalisia hali ya uchumi haiwezi kuwa nzuri kama Watanzania
wanalia kukosa fedha mtaani.
“Haiwezekani Watanzania wote walipata fedha kwa njia zisizo halali
kwa kuwa serikali imebadili mfumo wa ukusanyaji,” ilisema taarifa hiyo
na kumtaka gavana kuingilia kati na kuhakikisha fedha kwenye mzunguko
zinakuwepo ili wananchi waweze kuendesha maisha yao.
Mbunge wa Vunjo ambaye pia ni Mwenyekiti wa Chama cha NCCR-Mageuzi,
James Mbatia amemshauri gavana kuandaa mdahalo utakaowashirikisha wadau
mbalimbali wa masuala ya uchumi ili kujadili taarifa hiyo kwa kina kwa
kuona jinsi ukuaji huo wa uchumi utakavyosaidia mwananchi mmoja mmoja.
“Tunaposema uchumi unakua ni vyema tukaangalia pia, unasaidiaje
maisha ya mtu mmoja mmoja, je anaweza kupata kipato cha kula milo mitatu
kwa siku, je hali ya maisha ya Mtanzania wa kipato cha chini ikoje,
lazima ukuaji uchumi uakisi maisha ya watu hawa,” alisema Mbatia.
chanzo;habarileo.
Comments