VITAMBULISHO vya Taifa huenda vikatumika katika Uchaguzi Mkuu ujao wa Rais, Wabunge na Madiwani.
Hayo yalisemwa jana na Kaimu Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano wa
Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa (NIDA), Rose Mdami wakati akitoa
maelezo kwa Spika wa Bunge, Job Ndugai kwenye Ukumbi wa Pius Msekwa
bungeni mjini hapa katika hafla ya kumkabidhi kiongozi huyo wa Bunge
kitambulisho chake cha taifa.
Mdami alisema tayari mamlaka hiyo imechukua taarifa za wapigakura
kutoka kwenye kanzidata ya Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) na
kuzichakata na kuna uwezekano mkubwa vitambulisho vya taifa vikatumika
katika uchaguzi ujao na kuirahisishia kazi tume hiyo kufanikisha
uchaguzi huo wa Rais, Wabunge na Madiwani.
"Vitambulisho tunavyovitoa sasa vina saini ya mtu husika, hivyo
vitatumika benki. Tumewashirikisha pia NEC ambao wametupa 'database'
(kanzidata) yao, tumezichakata na tunaendelea na taratibu ili
ikiwezekana Vitambulisho vya Taifa vitumike katika Uchaguzi Mkuu wa 2020
badala ya vile vya tume," alisema Mdami.
Akishukuru, Ndugai aliipongeza mamlaka hiyo kwa kuwa na mipango
mizuri, lakini akaishauri serikali kuweka sharti kuzilazimisha benki
kutoruhusu mtu kufungua akaunti bila kuwa na kitambulisho cha taifa.
Spika pia alihoji sababu za Nida kuwa na vitambulisho vyenye rangi
tatu tofauti na kujibiwa na Mdami kuwa kitambulisho cha kwanza ni cha
raia mzawa, cha pili cha raia wa kigeni anayeishi nchi na cha mwisho kwa
ajili ya wakimbizi.
"Kwa sasa si rahisi mkimbizi kujichanganya mitaani huko na kupatiwa
kitambulisho cha taifa. Tunashirikiana na Tamisemi kuhakikisha hakuna
udanganyifu tena. Mtu anayejaza fomu ya kupatiwa kitambulisho anatakiwa
kupitia vipengele 72 ambavyo si rahisi kuvighushi kama si mzawa,"
alisema Mdami.
chanzo;habarileo.
Comments