VIONGOZI wa dini mkoani Kagera wameishauri serikali kushirikisha
wananchi katika mchakato mzima wa kutathmini madhara, yaliyotokana na
tetemeko la ardhi mkoani humo kwani mpaka sasa baadhi ya maeneo,
hayajafikiwa na kufanyiwa tathmini, huku wakiomba misaada kwa waathirika
iharakishwe.
Walitoa kauli yao jana wakati wakizungumza na gazeti hili katika
maeneo mbalimbali ya nyumba za ibada, yaliyoathirika kutokana tetemeko
hilo la Jumamosi wiki iliyopita ambalo lilisababisha vifo vya watu 17 na
kuacha wengine majeruhi zaidi ya 200 na kubomoa nyumba zaidi ya 1,000.
Askofu Msaidizi wa Kanisa Katoliki Jimbo la Bukoba, Methodius Kilaini
alisema wanapaswa kufanya tathmini mbili, kwanza ni ile ya haraka na
kuwatafutia watu maeneo ya kulala kama vile mahema, chakula na dawa.
Ya pili kufanya tathmini ya kuhusu majengo na kutafuta njia ya kupata vifaa vya ujenzi ili kujenga majengo au nyumba imara.
Kilaini, Askofu KKKT, Pentekoste wanena “Sisi kama viongozi wa dini
hatujaona watu wanakuja kufanya tathmini katika makanisa yetu
yaliyoathirika, nyumba za mapadri wanalala zimeanguka, wakitaka tathmini
ifanikiwe na kutoa majibu ya uhakika watushirikishe sisi jamii watu
wanataabika sasa mvua inakuja watu wanalala nje, wengine hawafikiwi na
wakiendelea hivyo bila kushirikisha jamii hali hiyo itachukua muda mrefu
huku watu wakiendelea kuathirika,” alisema Askofu Kilaini.
“Sisi tumepata hasara kubwa kutokana na hili janga, kanisa letu la
Ihungo limeharibika kabisa na kuanguka, nyumba ya kihistoria iliyojengwa
mwaka 1940 iliyokuwa ikitumiwa na mapadri katika kanisa hilo la Ihungo
imeanguka kabisa kwa hiyo lazima tujenge upya.
Kanisa la kihistoria
ambalo ni la kwanza mkoani Kagera lililojengwa mwaka 1892 na ndio
chimbuko la dini yetu hapa Bukoba pia limeharibika kabisa, tunahitaji
msaada wa haraka kulikarabati pia nyumba za mapadre pia zimeharibika
kabisa,” aliongeza Kilaini.
Alisema mpaka sasa mapadri wa sehemu hizo mbili, wanalala kwenye
magari, lakini jitihada za haraka zinafanyika za kuwajengea banda la
kujihifadhi wakati wakitafuta ufumbuzi wa kujenga makanisa hayo mawili
haraka kwani waumini wanasalia nje na hakuna mtu yeyote au taasisi
waliofika kutathmini kuhusu majanga yaliyowapata.
“Kwa sasa tuna kikao kuna kamati imetoka Baraza la Maaskofu (TEC) ili
kuona tunafanya nini kunusuru watu pia makanisa yetu mengine kumi
yamepata nyufa kubwa,” alisema Kilaini na kuiiomba serikali, wafadhili
mbalimbali kuwakumbuka wananchi wa Kagera walioathirika kwa kuwaletea
misaada ya haraka hasa mahema ili wajikinge na mvua na baridi, hili ni
janga limemgusa kila mmoja.
Askofu wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT) Dayosisi ya
Kaskazini Magharibi, Abedinego Keshomshahara katika tathmini ya mwanzo
waliyoifanya, wamegundua makanisa 10 kati ya 248 yamepata nyufa kubwa,
nyumba tatu za wachungaji zimepata nyufa, nyumba tano za wainjilisti
zimepata nyufa, na nyumba za watenda kazi wao 25 pia zimeharibika, na
hadi sasa hawajafanyiwa tathmini yoyote.
“Lakini hatuwezi kuilaumu serikali, hili tukio ni la ghafla kwani
kila mtu anakimbia huku na huku kuona ni vipi watawasaidia waliothirika
tunategemea tathmini kubwa itakuwa kwenye majumuisho ila la muhimu
wananchi washirikishwe ili kutoa takwimu sahihi kwani wao ndio
waathirika,” alisema Askofu Keshomshahara.
Naye Mwenyekiti wa Makanisa ya Kipentekoste, Mchungaji Edward
Crodward alisema tetemeko limeathiri makanisa mengi ila hawajamaliza
kufanya tathmini, ingawa tathmini ya mwanzo wamebaini makanisa saba
yamepata nyufa kubwa.
Kauli ya Shehe wa Mkoa Shehe wa Mkoa, Haruna Kichwabuta alitaja
athari walizozipata kutokana na tetemeko hilo kuwa ni misikiti mitatu
mikubwa iliyoko Manispaa ya Bukoba, imeanguka kabisa na kusababisha
kuifunga na hivyo waumini kuswalia nje, misikiti mingine minne imepata
nyufa kubwa, ofisi mbili za Bakwata zimepata nyufa na miundombinu ya
vyoo kuharibika.
Kichwabuta anashauri ifanyike tathmini ya kina bila kubagua wala
kutazama taasisi fulani ili kufanikisha kazi hiyo na kusaidia kwani wote
wanahitaji msaada wa haraka.
Wakati huo huo, wadau mbalimbali wameendelea kutoa misaada, na
Serikali ya China imetoa vifaa mbalimbali yakiwemo madawa, nguo, maji na
blangeti, Ubalozi wa Kuwait ukiwakilishwa na Shirika la African Muslim
wamekabidhi msaada wa Sh milioni 22 zikiwa Sh milioni 12 taslimu na
vifaa vya ujenzi na chakula vya Sh milioni 11, Serikali ya Zanzibar
imekabidhi Sh milioni 50 na Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Dayosisi ya
Kaskazini Magharibi ikitoa msaada wa chakula kwa waathirika hao.
Wabunge wachanga milioni 85.5
Mjini Dodoma, wabunge wamekusanya Sh 85,580,000 ili kusaidia
waathirika wa tetemeko la ardhi lililotokea mwishoni mwa wiki iliyopita
mkoani Kagera. Michango hiyo imetokana na uamuzi wa wabunge kuridhia
kuchangia posho zao za siku moja kila mmoja.
Hayo yalithibitishwa bungeni jana na Spika wa Bunge, Job Ndugai
alipokuwa akitoa taarifa za michango ya wabunge wa Bunge ambao kwa
ujumla idadi yao ni 389.
Wabunge hao, kwa kauli moja Jumanne wiki hii waliguswa na kuridhia
kutolipwa posho ya siku, kiasi cha Sh 220,000 kila mmoja ili zisaidie
waathirika wa tetemeko hilo lililosababisha vifo vya watu 17 na kujeruhi
zaidi ya watu 252.
Mashirika ya umma yatoa zaidi ya mil 800/- Jijini Dar es Salaam,
zaidi ya Sh milioni 800 zimechangishwa kutoka mashirika mbalimbali ya
umma na taasisi za serikali kupitia harambee maalumu ya kuchangia
waathirika wa tetemeko la ardhi lililotokea hivi karibuni mkoani Kagera.
Katika harambee hiyo iliyoongozwa na Msajili wa Hazina, Lawrence
Mafuru, pia baadhi ya mashirika yaliahidi kutoa mchango wao kwa njia ya
misaada ya kitaalamu kama vile wataalamu wa masuala ya ujenzi, wataalamu
wa jiolojia na mazingira.
Akizungumza katika mkutano maalumu, ulioandaliwa na ofisi ya Hazina
kwa ajili ya harambee hiyo Dar es Salaam jana, Mafuru alisema kutokana
na maafa makubwa yaliyosababishwa na tetemeko hilo kwa wakazi wa Kagera
ni jukumu la Watanzania wote kuungana na kutoa msaada kwa waathirika.
Aliyaomba mashirika hayo kuwasiliana na makatibu wakuu wao kupitia
wizara walizopo ili kuangalia namna ya kupunguza matumizi yao na
kuchangia waathirika hao wa tetemeko.
Katika michango hiyo iliyofikia zaidi ya Sh milioni 800, Kampuni ya
Tanzania Standard Newspapers (TSN) wachapishaji wa magazeti ya Daily
News, HabariLeo, HabariLeo Jumapili, Sunday News na SpotiLeo walichangia
jumla ya Sh milioni tano pamoja na matangazo bure kuhusu maafa hayo ya
Kagera kwa siku 30.
Meneja Uhusiano wa TSN, Badra Masoud aliyemwakilisha Mhariri Mtendaji
wa kampuni hii Dk Jim Yonazi, alisema pia Kampuni ya TSN ilirusha moja
kwa moja mkutano huo wa harambee kupitia tovuti za Daily News na
HabariLeo.
Shirika la Habari la Utangazaji Tanzania (TBC), nalo lilichangia
kiasi cha Sh milioni tano kutoa matangazo bure yanayohusu maafa hayo na
kurusha mkutano huo wa harambee ya kuchangia waathirika hao moja kwa
moja.
Baadhi ya kampuni, mashirika na taasisi nyingine za umma
zilizochangia katika harambee hiyo ni Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania
(TCRA) (milioni 60), Benki Kuu ya Tanzania (BoT) (milioni 50), Mamlaka
ya Bandari Tanzania (TPA) (milioni 50) na Benki ya Rasilimali Tanzania
(TIB) (milioni 25).
Wengine waliochangia ni Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania
(TPDC) (milioni 20), Mamlaka ya Hifadhi za Taifa (Tanapa) (milioni 20),
Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS) (milioni 20), Shirika la Umeme
Tanzania (Tanesco) (milioni 15), Mamlaka ya Usafiri wa Nchi Kavu na
Majini (Sumatra) (milioni 10) na Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya NHIF
(milioni 10).
Aidha taasisi, mashirika na kampuni nyingine za umma zilizochangia
katika harambee hiyo ni Mamlaka ya Usafiri wa Anga Tanzania (TCAA)
(milioni 10), Benki ya Posta Tanzania (TPB) (milioni 10), Chuo cha Taifa
cha Usafirishaji (NIT) (milioni 10), Wakala wa Majengo Tanzania
(milioni 10) na Mamlaka ya Udhibiti wa Bima Tanzania (milioni 10).
Nyingine zilizochangia Sh milioni tano ni ofisi ya Msajili wa Hazina,
Bodi ya Tumbaku (TTB), Baraza la Taifa la Uhifadhi na Usimamizi wa
Mazingira (NEMC), Chuo cha Mafunzo ya Ufundi Stadi na Huduma (VETA),
Bodi ya Usajili wa Makandarasi na Chuo cha Bahari (DMI). Udsm, MSD, DIT,
JKT kutoa utaalamu Aidha, Chuo Kikuu cha Dar es Salaam kilisema kimetoa
mchango wa kupeleka wataalamu wake wa masuala ya jiolojia mkoani Kagera
ambao pamoja na kuendelea na utafiti kupitia kituo cha kufuatilia
matetemeko kilichopo mkoani Geita, pia watafungua kituo mkoani Kagera
kufuatilia zaidi hali ya matetemeko.
Kwa upande wa Bohari ya Dawa Tanzania (MSD) yenyewe imeahidi
kusambaza dawa kwa waathirika hao zenye thamani ya Sh milioni 30, Chuo
cha DIT kiliahidi kutoa msaada wa kitaalamu zaidi katika maeneo
yaliyoathirika na Jeshi la Kujenga Taifa (JKT) nalo litatoa askari wake
kwa ajili ya ujenzi.
Mapema wiki hii, Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa, pia aliitisha harambee
ya wafanyabiashara kwa ajili ya kuchangia waathirika hao wa tetemeko na
jumla ya Sh bilioni 1.4 ziliahidiwa kutolewa pamoja na misaada ya
ujenzi wa taasisi mbalimbali ikiwemo shule zilizoathirika.
Aidha, serikali ilisema inalichukulia suala hilo kwa ukubwa wake na
ndio maana, Rais John Magufuli aliahirisha safari ya kikazi Lusaka,
Zambia kuhudhuria sherehe za kuapishwa kwa Rais wa nchi hiyo, Edgar
Lungu.
Wajenzi waombwa vifaa Nayo Idara ya Maafa Ofisi ya Waziri Mkuu
imeomba viwanda vinavyozalisha vifaa vya ujenzi, watoe msaada wa
kuzalisha vifaa maalumu vyenye nembo Kagera na bei ndogo, ili
vikawezeshe waathirika wa tetemeko Bukoba wajenge nyumba zao haraka.
Akizungumza jana jijini Arusha, Mkurugenzi Idara ya Maafa Ofisi ya
Waziri Mkuu, Brigedia Jenerali Mbazi Msuya katika mafunzo ya siku mbili
ya wanahabari, mashirika yasiyo ya kiserikali na Asasi za Kiraia ya
kuwajengea uwezo masuala ya maafa, alisema vifaa hivyo vizalishwe ndani
ya miaka miwili.
Alisema kama bati au mfuko wa saruji ni vyema kuandikwa jina Kagera
ili usiuzwe kokote ni huko na bei iwe ndogo, lakini sio hivyo tu ni
vifaa vyote vya ujenzi vya Kagera. Aliomba wazalishaji washushe bei ya
vifaa hivyo iwe chini na wasisingizie kodi ili kusaidia waathirika hao.
Aidha, alisema mpaka jana wagonjwa waliopo wodini 53 kati yao 21
wameshaonwa na madaktari bingwa kutoka China na baadhi watafanyiwa
upasuaji.
Mwinyi kuongoza matembezi Naye Rais mstaafu wa Awamu ya Pili, Ali
Hassan Mwinyi kesho ataongoza matembezi ya hiari ya kilometa tano,
kuchangisha fedha kuwasaidia wananchi walioathirika na tetemeko la ardhi
lililotokea mwishoni mwa wiki iliyopita mkoani Kagera.
Matembezi hayo yaliyoandaliwa na Wizara ya Mambo ya Nje na
Ushirikiano wa Afrika Mashariki, yatashirikisha jumuiya ya
wanadiplomasia, mawaziri, makatibu wakuu pamoja na wananchi.
Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano ya Serikali na Msemaji wa Wizara ya
Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mindi Kasiga alisema
matembezi hayo yataanza saa 12 asubuhi katika Bwalo la Maofisa wa Polisi
Oysterbay.
Kasiga alisema kiingilio katika matembezi hayo ni Sh 10,000, lakini
wananchi wa kawaida wanaalikwa kuingia kwa fedha yoyote waliyonayo.
Alisema wanahamasisha kampuni, benki na taasisi mbalimbali kujitokeza
kuchangia. Fedha zitakazopatikana zitapelekwa katika akaunti
iliyofunguliwa na Ofisi ya Waziri Mkuu.
Imeandikwa na Angela Sebastian (Bukoba), Veronica Mheta (Arusha),
Eric Anthony (Dodoma) na Theopista Nsanzugwanko na Halima Mlacha (Dar).
chanzo;habarileo.
Comments