Katika kuhakikisha watoto wa kike
wanakuwa shuleni na hatimaye kumaliza masomo yao, Shirika la Umoja wa
Mataifa la Elimu, Sayansi na Utamaduni (UNESCO) limetenga Dola 1,605,000
ambazo ni zaidi ya Bilioni 3 za Kitanzania ambayo zitatumika kuwasaidia
watoto wa kike nchini kurejea katika shuleni kwa ajili ya kuendelea na
masomo.
Akizungumzia mradi huo, Mkuu wa Ofisi na Mwakilishi wa
UNESCO nchini, Bi. Zulmira Rodriguez alisema kuwa Tanzania bado
inaonekana kuwa na tatizo la watoto wa kike kuachishwa masomo yao
kutokana na sababu mbalimbali ikiwepo kupata mimba za utoto na ndoa za
utotoni hivyo kupitia mradi huo wataweza kuwasaidia watoto hao kuendelea
na masomo.
Bi. Rodriguez alisema UNESCO imeamua kushirikiana na
serikali ya Tanzania ili kuwasaidia watoto wa kike kurejea masomoni na
utafanyika kwa uhakika bila kumwacha mtoto yoyote na wana matumaini
utaweza kusaidia watoto wa kike ambao wamekatishwa ndoto zao kimaisha
kutokana na kukatishwa masomo.
"Tanzania kuna tatizo la watoto wa
kike kusahaulika katika elimu na UNESCO imejitoa kushirikiana na
serikali ya Tanzania ili kusaidia kukuza elimu ya watoto wa kike,
"Baadhi ya mambo ambayo yanaonekana kuchangia ni pamoja na mambo ya
asili, wamekuwa wakiwaozesha ndoa za utotoni na na watoto wengine
wamekuwa wakipata mimba za utoto na hivyo kuacha masomo … mradi huu ni
wa uhakika na utasaidia kukuza elimu," alisema Bi. Rodriguez.
Kwa
upande wa Katibu Mkuu wa Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, Bi.
Maimuna Tarishi alisema serikali inafahamu kuwepo kwa changamoto hizo na
imekuwa ikifanya jitihada ili kuhakikisha kuwa matatizo ya watoto wa
kike kukatishwa masomo yakimalizika.
Alisema kuwa makabila mengi
ya Tanzania yamekuwa yakiwaona watoto wa kike kama watu wa kukaa
nyumbani na kulea watoto lakini kama jamii ikiwa na mtizamo tofauti na
kuwawezesha watoto wa kike basi wanaweza kusaidia nchi kukuza uchumi.
"Tumeona
kazi ambayo wameifanya UNESCO hata machifu huko Ngorongoro wameanza
kuelewa umuhimu wa watoto wa kike kuwa shuleni na kwa mpango huu
matarajio ya serikali ni kumaliza changamoto iliyokuwepo awali,
"Serikali
inafahamu kuna changamoto nyingi ambazo zinawakuta watoto wa kike na
sio katika elimu pekee bali ni maeneo mengi … serikali inataka kukuza
thamani ya elimu kwa watoto wa kike ambao wengi wao wanakatishwa kwa
sababu ya mimba na ndoa za utotoni," alisema Bi. Tarishi.
Nae
Afisa Mradi wa Maswala ya Afya ya Uzazi kwa Vijana (UNFPA), Fatina
Kiruviya alisema mradi una malengo ya kuhakikisha watoto wa kike
wanakuwa shuleni na kwa kuanza wanataraji kufanya mradi Ngorongoro,
Pemba, Geita na Sengerema.
chanzo;bbc.
Comments