Sera ya Diaspora kufikishwa Baraza la Wawakilishi.


Image result for jengo la baraza la wawakilishi zanzibar

WAZIRI wa Nchi, Ofisi ya Rais na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Issa Haji Gavu, amesema Sera ya Diaspora ipo katika hatua ya mwisho kupelekwa katika Baraza la Wawakilishi.

Gavu amesema hayo wakati alipozungumza na gazeti hili akielezea juhudi zinazochukuliwa na Ofisi ya Rais kuhusu Sera ya Wazanzibari wanaoishi nje ya nchi (Diaspora) ambayo imechukua muda mrefu huku jamii hiyo ikisisitiza kutayarishwa ili iweze kutoa mchango wake katika taifa.

Amesema sera hiyo ambayo imechukua takribani miaka mitatu kujadiliwa na kupitiwa pamoja na serikali kupokea maoni tofauti kutoka kwa wadau na sasa imepitishwa na kujadiliwa katika ngazi ya makatibu wakuu.

“Sera ya Diaspora tayari ipo katika hatua nzuri imepitishwa na makatibu wakuu na sasa inatarajiwa kwenda katika ngazi ya Baraza la Mapinduzi kwa hatua za mwisho kabla ya kufikishwa mbele ya Baraza la Wawakilishi,” amesema Gavu.

Amesema Sera hiyo ni muhimu kwa sababu ndiyo muongozo ambao utawawezesha Watanzania wanaoishi nje ya nchi kuchangia maendeleo ya taifa kikamilifu katika sekta mbalimbali pamoja na jamii hiyo kutambuliwa na serikali.

Gavu alisema Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar imejizatiti kuona kwamba sera hiyo inakamilika na kuwasilishwa mbele ya Baraza la Wawakilishi kwa ajili ya utekelezaji wake na ndio maana hivi karibuni Zanzibar ilikuwa mwenyeji wa mkutano wa tatu wa Diaspora kitaifa.

Hivi karibuni katika Mkutano wa Kimataifa wa Diaspora uliofanyika Zanzibar, Rais wa Zanzibar, Dk Ali Mohamed Shein alizitaka taasisi zinazohusika na masuala ya Diaspora, kuharakisha kukamilisha sera hiyo ili wahusika wachangie maendeleo ya taifa.

chanzo;habarileo.

Comments