Rais Magufuli atoa siku 7 kwa Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano kumaliza deni wanalodaiwa na NHC
Rais
wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli
ametoa siku 7 kwa Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano kulipa deni
la bilioni 2 ambalo wanadaiwa na Shirika la nyumba la Taifa (NHC).
Dkt.
Magufuli ametoa agizo hilo kwa Katibu Mkuu wa Sekta ya Ujenzi, Injinia
Joseph Nyamhanga leo jijini Dar es Salaam katika ziara ya kushtukiza ya
kuangalia ujenzi wa hosteli za wanafunzi wa Chuo Kikuu cha Dar es
Salaam.
“Nawapa
siku 7 muwe mmelilipa hilo deni huku mkiendelea na utaratibu wa kuhamia
Dodoma, kama hamtalilipa kwa wakati nitawaagiza NHC kuwatolea vitu
vyenu nje kama wanavyofanya kwa wengine,” alisema Dkt. Magufuli.
Amesema
kuwa kiwango hicho cha bilioni 2 kingeiwezesha wizara hiyo kujenga
ofisi za wizara kwa kuwatumia Wakala wa Majengo (TBA) ambao wako chini
ya wizara hiyo badala ya kutumika kama kodi ya pango.
Aidha,
ameitaka wizara hiyo kuhamia Mjini Dodoma mara tu watakapokamilisha
deni hilo na kutoendelea kupanga jijini Dar es Salaam, kwani hakuna
sababu ya kuendelea kupanga majengo ya ofisi Dar es Salaam wakati
Serikali yote inahamia Dodoma.
Wakati
huohuo, Rais Dkt. Magufuli ameipongeza Wizara ya Elimu, Sayansi na
Tecknolojia, Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano pamoja na Wakala
wa Majengo (TBA) na uongozi wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam kwa
kusimamia vizuri mradi wa ujenzi wa hosteli za chuo kikuu ambao Rais
mwenyewe aliahidi shilingi bilioni 10 katika ujenzi huo, bilioni 5
imekwishatolewa na bilioni nyingine 5 itatolewa ndani ya wiki hii.
Hosteli
hizo zinategemea kuchukua wanafunzi 4000 ambapo itapunguza kwa kiasi
kikubwa tatizo la wanafunzi kukaa nje ya maeneo ya chuo.
chanzo;mpekuziblog.
Comments