WATANZANIA wameshauriwa kutumia fursa zinazopatikana katika chuo
kipya cha kilimo cha Borigam, kilichojengwa kwa msaada wa Korea, ili
kupata utaalamu zaidi kuhusu kilimo.
Akizungumza katika hafla ya ufunguzi wa chuo hicho kilichojengwa kwa
msaada wa Jumuiya ya Wabudhi katika wilaya ya Kigamboni jijini Dar es
Salaam, Naibu Waziri wa Kilimo, Mifugo na Uvuvi, William ole Nasha,
alisema kujengwa kwa chuo hicho cha kilimo cha matunda na mboga ni fursa
kubwa itakayowezesha kuongeza idadi ya maofisa ugani.
“Hii ni fursa kwa wakazi wa Kigamboni, Dar es Salaam na Tanzania,
tuitumie kuhakikisha tunaongeza wataalamu wengi zaidi katika sekta ya
kilimo cha matunda na mboga,” alisema Ole Nasha. Alisema vipo vyuo vya
kilimo 14 nchini, lakini vinavyofundisha kilimo cha mboga na matunda ni
vichache.
Alisema nchi inahitaji maofisa ugani 20,000 lakini waliopo ni nusu ya
idadi hiyo, hivyo anaamini chuo hicho kimekuja kwa wakati muafaka
kutatua changamoto hiyo.
Mkuu wa chuo hicho kilichopo Mwasonga katika wilaya mpya ya
Kigamboni, Joseph Ndunguru, alisema kitasaidia kuzalisha maofisa ugani
wengi zaidi katika kilimo cha mboga na matunda.
Mbali na kutoa mafunzo kwa wanachuo, pia kitatoa mafunzo kwa wanakijiji wa eneo hilo kuhusu kilimo hicho.
Alisema wamezungumza na uongozi wa shule ya msingi Mkamba uliotoa
hekta 10 za ardhi zitakazotumika kama shamba darasa kwa wanafunzi
watakaokuwa wakisoma katika chuo hicho na pia kwa wanakijiji kujifunza.
Alisema kujiunga na chuo hicho ni bure kwa kuwa gharama zote
zimelipwa na wafadhili. Alitaja gharama hizo kuwa ni za chakula, malazi
na masomo na kuongeza kuwa mwanafunzi atapaswa kulipia mafunzo kwa
vitendo pekee.
chanzo;habarileo.
Comments