MWENYEKITI wa Tanzania Labour Party (TLP), Augustino Mrema,
amempongeza Msajili wa Vyama vya Siasa nchini, Jaji Francis Mutungi kwa
jitihada za kusuluhisha mgogoro wa uongozi uliokuwepo ndani ya Chama cha
Wananchi (Cuf).
Amewasihi viongozi wengine wa vyama vyote vya siasa nchini kuzingatia
Katiba za vyama vyao, misingi ya demokrasia na sheria za nchi, ili
kuepusha na kuondoa migogoro ndani ya vyama au kati ya chama kimoja na
kingine.
Amesema hakuna kiongozi wa kisiasa aliyekamilika kwa asilimia 100
kwakuwa , kila mmoja ana udhaifu wake. Mrema alitoa pongezi hizo jana
Dar es salaam kupitia taarifa yake kwa vyombo vya habari. Sehemu ya
taarifa hiyo ilisema, " TLP inampongeza Msajili na ofisi yake kwa
kutatua mgogoro huo kwa kuzingatia sheria za nchi, sheria ya vyama vya
siasa na pia, imezingatia misingi ya demokrasia ambayo ni nguzo ya mfumo
wa vyama vingi vya siasa".
Alisema chama hicho kinaamini kuwa ofisi ya Msajili wa Vyama vya
Siasa haikupendelea upande wowote kama baadhi ya watu wanavyodai, bali
imefanya kazi yake kwa kuzingatia sheria ya vyama vya siasa ambayo kwa
mujibu wa mamlaka aliyopewa Msajili na sheria hiyo kukifuta chama
chochote cha siasa nchini, endapo kitakwenda kinyume cha sheria hiyo,
pamoja na kusuluhisha migogoro.
Alisema kwa vile ofisi ya Msajili imeshatoa maelekezo kwa chama cha
Cuf, ni vyema wanachama wote wa chama hicho wakatulia na kutekeleza
maagizo yaliyotolewa na ofisi hiyo, ili kupata suluhisho la kudumu kwa
manufaa ya chama chao na kwa manufaa ya taifa.
Alitumia muda huo kuwataka viongozi wa vyama vya siasa nchini
kuzingatia Katiba za vyama vyao, misingi ya demokrasia na sheria za nchi
ili kuepusha na kuondoa migogoro ndani ya vyama au kati ya chama kimoja
na kingine au Serikalini.
“Nasema hivyo kwa sababu wapo baadhi ya viongozi wa vyama vya siasa
wamekuwa mstari wa mbele kumlaumu Rais John Magufuli kwamba anavunja
Katiba ya nchi pia, wanadai kwamba anavunja sheria za nchi na misingi ya
demokrasia wakati wao wenyewe ndio vinara wakuvunja Katiba za vyama
vyao na sheria za nchi pamoja na misingi ya demokrasia,” alisema.
Alitoa mfano chama kimoja cha siasa ambacho kiliendesha vikao vya
kitaifa, lakini idadi ya wajumbe wa vikao hivyo haikulingana na uwiano
halisi wa idadi ya wanachama wa chama hicho waliokuwepo kwenye pande
mbili za muungano.
Mrema alisema kutokana na pongezi hizo wapo watakaosema kwa nini yeye
(Mrema) apongeze ilhali alisababisha migogoro ndani ya vyama vya NCCR –
Mageuzi na TLP? Akitetea, alisema hakuna kiongozi wa kisiasa
aliyekamilika kwa asilimia mia 100, kila kiongozi anaudhaifu wake,
lakini hata hivyo hakuwahi kufanya makosa makubwa kama wanayofanya
wenzake.
“Sijawahi kuitisha vikao ambavyo idadi ya wajumbe hailingani na
uwiano halisi wa wanachama wa chama changu waliopo Tanzania Bara na
Zanzibar,” alisema na kuongeza kuwa hajawahi kubadilisha Katiba ya chama
chake kinyemela ili aweze kuendelea kubakia madarakani.
Alimtaka Msajili asikubali kuyumbishwa au kushinikizwa na kikundi
chochote kile kwa manufaa au maslahi ya watu fulani, huku akimhimiza
kuendelea kulinda sheria ya vyama vya siasa na misingi ya demokrasia na
kwamba asisite kukichukulia hatua zinastahili chama chochote
kitakachokiuka mambo hayo kama ambavyo ofisi hiyo ilivyopewa mamlaka kwa
mujibu wa sheria ya vyama vya siasa.
chanzo;habarileo.
Comments