Taasisi ya Siti Binti Sadi yachangiwa mil 800/- .

RAIS wa Zanzibar, Ali Mohamed Shein amechangia Sh milioni 50 katika harambee ya kuchangisha fedha kwa ajili ya jengo la taasisi ya Siti Binti Sadi. Alisema kuwa msanii huyo Siti Binti Sadi anastahili kujengewa jengo maalumu kwa ajili ya kumuenzi na watu wa nje wafike kuona.


Rais Shein alitoa kauli hiyo juzi usiku katika harambee hiyo iliyofanyika katika hoteli ya Park Hayat visiwani hapa.

Alisema kwamba katika safari yake ya harakati za kuimba, msanii huyo alikutwa na misukosuko mingi ikiwemo watu kumkejeli kwa wimbo na kwa mashairi.

Hivyo alisema kwamba ujenzi wa jengo hilo utatoa fursa ya kuzidi kutambulika kwa kazi za msanii huyo kutokana na watu wengi kufika na kusoma historia yake na kutambua mahala alipozaliwa. Alisema kwamba wana jukumu la kila fani nao kumtuza kutokana na mchango wake mkubwa alioutoa katika kuipa heshima nchi yao.

“Ni wajibu wa kuitunza ajira yake na maisha yake, Siti alifanya kazi kubwa katika kukitangaza Kiswahili na Kiswahili alichokitumia kile cha hali ya juu katika nyimbo zake, ambapo kwa sasa hatuwezi kukipata," alisema.

Hata hivyo, alisema Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar inafanya uwazi wa kuwaenzi waimbaji wote wakongwe na wa sasa. Siti Binti Sadi alizaliwa mwaka 1870 katika kijiji cha Fumba, ambapo ndipo kutajengwa jengwa hilo na kufariki dunia mwaka 1950 na kuzikwa Rahaleo.

Katika harambee hizo jumla ya sh milioni 800 zilipatikana zikiwemo ahadi, ambapo Rais wa Zanzibar akichangia Sh milioni 50.

chanzo;habarileo.

Comments