Mamlaka
ya Mapato Tanzania(TRA) imekamata akaunti za Kampuni ya Sahara Media
Group kwa kushindwa kulipa deni la Sh4 bilioni kama kodi iliyopaswa
kulipwa na kampuni hiyo.
Taarifa
zilizosambaa kupitia mitandao ya kijamii zimeeleza kuwa akaunti zote za
kampuni hiyo zimefungiwa mpaka pale watakapolipa deni hilo, lakini
kampuni hiyo imetoa ufafanuzi.
Ujumbe
huo uliongeza kuwa kampuni hiyo imefikishwa mahakamani na benki moja
hapa nchini kwa madai ya kutaka kulipwa Sh600 milioni, baada ya kuingia
makubaliano ya kulipa wafanyakazi wake mishahara pamoja na mikopo
lakini mpaka sasa imeshindwa kurejesha fedha hizo.
Hata
hivyo, akizungumzia suala hilo mwenyekiti mtendaji wa kampuni ya
Sahara, Anthony Diallo alikiri mamlaka hiyo kufungia akaunti ya kampuni
yake.
Diallo
ambaye ndiye mmiliki wa kampuni hiyo alisema ni akaunti moja tu
iliyofungiwa na kwamba anaamini baada ya kukutana na kufanya mazungumzo
na mamlaka hiyo watafikia muafaka ili biashara ziendelee kama kawaida.
“Tutalimaliza hakuna kitakachoenda mrama,” alisisitiza
Diallo ambaye aliwahi kushika nyadhifa mbalimbali serikalini ikiwamo
nafasi ya Waziri wa Maliasili na Utalii na Naibu Waziri wa Maji,
Maendeleo ya Mifugo katika Awamu ya Nne chini ya Rais mstaafu Jakaya
Kikwete.
Amesema deni la TRA linatokana na kodi iliyopatikana baada ya ukaguzi wa vitabu kwa miaka mitatu.
“Ni
ukaguzi wa kawaida hufanyika kama taratibu. Sasa kwa sababu ya
kuhamisha matangazo yetu kutoka analojia kwenda digitali ilibidi tukope
benki, ujenzi na kumaliza mradi imechukua miaka mitatu. Wakati wote
tumekuwa tukilipa riba benki na zinazobaki toka mauzo ya matangazo
tunalipa mishahara, umeme na malipo ya kodi za kawaida,”alisema.
“Ni
kawaida ila wamefanya hatua za kutuaibisha tu. Kampuni yetu ya
ving’amuzi ni ya Kitanzania na mapato yote yanaingia nchini wakati
kampuni nyingine kubwa zote ni za kigeni kutoka China, Afrika Kusini,
Mauritius na Kenya! Ukweli sisi tunahitaji kusaidia nchi kiuchumi na
kutuharibia ni hasara kwa nchi.”
chanzo;mpekuziblog.
Comments