WAZIRI wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais (Mazingira na Muungano),
January Makamba amesema tangu nchi ipate Uhuru miaka 50 iliyopita,
maadui watatu ambao ni maradhi, umasikini na ujinga wapo pale pale, hali
inayofanya kuwe na tofauti kubwa kati ya walichonacho na wasichonacho.
Aidha, amesema ameongezeka adui mwingine wa nne ambaye ni tofauti kubwa ya usawa kati ya walichonacho na wasichonacho.
Makamba alisema jana jijini Dar es Salaam alipokuwa akizindua ripoti
ya hali ya kipato cha uchumi Afrika Mashariki iliyotolewa na Taasisi ya
Society for International and Development (SID).
Alisisitiza kuwa, kama nchi inataka kujenga taifa la watu walio sawa
hakuna budi kukabiliana na suala hilo, kwani usawa katika fursa ndiyo
nyenzo muhimu ya kukabiliana na usawa katika jamii.
“Katika safari ya nchi yetu tumepata wazungu wapya ambao ni Waafrika
wenzetu. Watu wanaishi maisha mazuri sana, watoto wao wanapata elimu
nzuri sana, sasa hivi tofauti imekuwa ni kubwa sana,” alisema Makamba.
Makamba alisema moja ya misingi ya ujenzi wa taifa letu ni umoja na
usawa ambao ni tunu iliyopo katika taifa, hivyo usawa unapotishiwa na
tofauti kubwa ya kipato ama kupata huduma, walichonacho na wasichonacho,
ni wajibu wa viongozi wa siasa kuliangalia suala hilo kwa uzito.
Alisema ni jukumu la viongozi kuhakikisha ubora wa elimu unaboreshwa
kwa kuwa hivi sasa kuna tofauti kubwa ya kiwango cha ubora wa elimu
kinachotolewa kwa watoto wa Tanzania.
“Kama mbunge katika jimbo langu naona watoto wanakaa chini, chakula
hamna, walimu hawana nyumba za kuishi, lakini ukija mjini ni tofauti.
Kwa hili tu umeshatengeneza mataifa mawili tofauti…tunaingia katika
ulimwengu wenye ushindani mkubwa, elimu pekee ndiyo itakayosaidia watoto
wetu,” alisema.
Alisema ripoti hiyo itaanzisha mjadala muhimu juu ya usawa, hivyo
kila mmoja anapaswa kushiriki. Naibu Mkurugenzi Mtendaji wa SID, Arthur
Muliro alisema ripoti hiyo imeangalia sekta nyingi ikiwemo elimu na
usalama, matokeo waliyonayo hayaoneshi kama kuna usawa.
chanzo;habarileo.
Comments