MAMENEJA wawili wanaosimamia Kituo cha Kupozea Umeme cha Kurasini,
Dar es Salaam wamesimamishwa kazi kutokana na kutokamilisha ujenzi wa
kituo hicho.
Aidha, Meneja Miradi wa Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco), Emmanuel
Manirabona ametakiwa kutoa maelezo ni kwa nini kituo hicho
hakijakamilika tangu kilipoanza kujengwa mwaka 2012 na kutakiwa
kukamilika Novemba, 2013.
Hayo yalibainishwa jana Dar es Salaam na Naibu Waziri wa Nishati na
Madini, Dk Medard Kalemani wakati alipotembelea vituo vya kupozea umeme
vya Kurasini, Mbagala na Gongo la Mboto ambavyo ujenzi wake
haujakamilika.
Dk Kalemani alisema kutokukamilika kwa vituo hivyo ndio kunasababisha
kuendelea kwa tatizo la umeme jijini Dar es Salaam hivyo aliagiza
ifikapo Septemba mwaka huu, jiji hilo liwe linapata umeme wa uhakika
kutoka katika vituo vyake vitatu ili kuondoa tatizo la kukatika kwa
umeme mara kwa mara.
Alisema katika vituo hivyo, kazi zimeonekana kusuasua kutokana na
watendaji wa Tanesco kukaa ofisini pekee bila kufuatilia maendeleo ya
mradi huo.
Alisema Tanesco wanatakiwa kukamilisha ujenzi wa vituo hivyo pamoja
na kuunganisha umeme kutoka Gongo la Mboto hadi Mbagala ifikapo Septemba
mwaka huu ili kuwa na umeme wa kutosha.
“Miradi hii ilianza mwaka 2012 na ilitakiwa kuchukua miezi 18 pekee,
yaani hadi 2013 iwe imekamilika. Lakini mpaka sasa kituo cha Kurasini
hakuna kinachoendelea na meneja wake hayupo kazini. Mameneja wa kituo
hiki cha Kurasini wasimamishwe…nikija Jumanne nikute meneja wengine na
wewe ambaye ni Meneja Miradi hadi ifikapo Jumanne (wiki ijayo) uwe
umeandika barua ya kujieleza ni kwa nini mradi umecheleweshwa. Pia
tutachunguza kiasi cha fedha kilichotumika kwenye mradi na kazi
iliyofanywa.”
Meneja wa Miradi, Manirabona alisema Kituo cha Kurasini kilitakiwa
kianze kujengwa mwaka 2012 na kukamilika Novemba 2013, lakini mpaka sasa
wanasubiri vifaa.
Alisema mkandarasi alipewa malipo yake kwa asilimia 80 na kwamba kazi
aliyoifanya ni sawa na asilimia 50, lakini tangu Machi mwaka jana
mkandarasi hayupo kituoni hapo.
Alieleza kuwa katika Kituo cha Mbagala walitarajia kuanza kupokea
umeme kutoka Gongo la Mboto, Desemba mwaka huu na kwamba kesi iliyokuwa
mahakamani ndio iliweka zuio la kuendelea kwa kituo hicho, lakini kesi
ilimalizika Mei mwaka huu.
chanzo;habarileo.
Comments