Wakadiriaji majenzi watakiwa kuzingatia maadili ya kazi zao.

MAKAMU wa Rais, Samia Suluhu Hassan, amewataka wakadiriaji majenzi nchini wahakikishe wanafanya kazi kwa kuzingatia maadili na waepuke vitendo vya rushwa katika mchakato wa ukadiriaji majengo nchini.

Alitoa agizo hilo jana wakati akifungua mkutano wa mwaka wa wakadiriaji majenzi kutoka nchini mbalimbali za Afrika jijini Dar es Salaam.

Alisisitiza kuwa kwa sasa serikali ipo kwenye mchakato wa kuanza kutekeleza miradi mikubwa ya kiuchumi ikiwemo ujenzi wa reli ya kati kwa kiwango cha kisasa na ujenzi wa bomba la mafuta kutoka nchini Uganda hadi Tanga.

Pia, alitaja suala la kuhamishia Makao Makuu Dodoma na kusema kuwa ni muhimu kwa wakadiriaji majenzi kujipanga vizuri kutekeleza miradi hiyo kwa kuweka gharama nafuu kulingana na hali halisi ya mradi unaotakiwa kujengwa.

Alisema serikali inatambua mchango wa wataalamu wa ukadiriaji majenzi hivyo ni muhimu wakaongeza bidii katika utekelezaji wa kazi zao hasa kwa kuzingatia teknolojia za kisasa.

Samia alihimiza ushirikiano kati wakadiriaji majenzi wa Tanzania na wa nchi nyingine za Afrika katika kubadilishana uzoefu, ili kuongeza ubunifu na ufanisi katika miradi wanayopata.

Kwa upande wake, Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Profesa Makame Mbarawa alisema serikali imetenga Dola za Marekani bilioni 2.4 kwa ajili ya utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo, ukiwemo ujenzi wa barabara, madaraja na bandari na viwanja wa ndege hivyo serikali inahitaji wakadiriaji majenzi waadilifu katika utekelezaji wa miradi hiyo.

chanzo;habarileo.

Comments