SIKU moja baada ya wilaya ya Arusha na Halmashauri ya wilaya ya
Kinondoni, Dar es Salaam kubaini uwepo wa wanafunzi hewa waliopata mgawo
wa fedha za elimu bure, Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Anthony Mtaka naye
amebaini wanafunzi wa aina hiyo wapatao 2,331 mkoani mwake.
Uwepo wa wanafunzi hao unaashiria moja kwa moja ulaji fedha
zilizotengwa na Rais John Magufuli alizotenga kwa ajili ya kugharimia
elimu bure kwa wanafunzi wa shule za msingi na sekondari nchini.
Akizungumza kwa njia ya simu jana, Mtaka alisema kutokana na taarifa
za awali za kuwepo kwa wanafunzi hewa, ameagiza kuvuliwa vyeo kwa walimu
wote wakuu wa shule hizo, lakini pia wanaandaa mpango maalumu wa
kuwafanyia uhakiki walimu wote wakuu ili kujua tabia na mienendo yao
kabla ya kuwapa wadhifa huo.
Alisema katika uhakiki wa wanafunzi kwa shule za msingi na sekondari
mkoa mzima, taarifa za awali zimeonesha mpaka sasa katika shule za
sekondari wamebainika kuwepo wanafunzi hewa 2,331 na bado unaendelea na
pindi ukikamilika atatoa taarifa kamili.
Alisema kwa upande wa shule za msingi, kazi inaendelea na upande wa
shule za sekondari wilaya pekee ambayo haikuwa na wanafunzi hewa ni
Bariadi huku wilaya ya Itilima ikiwa na wanafunzi hewa 2,137, Meatu 121,
Busega 110 na Maswa imebainika kuwa na wanafunzi hewa 14 na kazi ya
uhakiki bado inaendelea.
“Mkoa wa Simiyu una jumla ya shule za msingi za serikali 516 na shule
za sekondari 140, ambapo jumla ya walimu wakuu wa shule zote wapatao
656 watavuliwa madaraka yao kuanzia sasa,” alisema Mtaka aliyemwagiza
Katibu Tawala wa Mkoa huo, Jumanne Sagini kuwavua madaraka mara moja
wakuu wote 140 wa shule za sekondari mkoani humo kutokana na kugundulika
uwepo wa wanafunzi hewa.
chanzo;habarileo.
Comments