SERIKALI imeamua kukata rufaa katika Mahakama ya Rufani dhidi ya
uamuzi wa Mahakama Kuu uliosema kipengele cha umri wa mtoto wa kike
kuolewa chini ya miaka 18 kwamba kinakiuka Katiba kwa nia ya kuufanya
uamuzi huo kuwa sheria.
Uamuzi wa Mahakama Kuu uliitaka Serikali kufuta vifungu viwili cha 13
na 17 vya Sheria ya Ndoa ya Mwaka 1971 vinavyoeleza mtoto wa miaka 14
na 15 anaweza kuolewa kwa idhini ya mzazi au Mahakama.
Waziri wa Katiba na Sheria, Dk Harrison Mwakyembe alisema kuwa
Serikali imeamua kukata rufaa Mahakama ya Rufani dhidi ya uamuzi huo si
kupinga uamuzi wa Mahakama Kuu, bali kupata uamuzi wa chombo cha juu cha
Mahakama ambao hautaweza kubadilishwa na hivyo kuwa kama sheria.
Aliyasema hayo jana Dar es Salaam alipokutana na Chama cha Wanasheria
Wanawake Tanzania (TAWLA) ambao walimtembelea ofisini kwake kuzungumzia
mambo kadhaa likiwemo suala hilo la serikali kukata rufaa dhidi ya
hukumu hiyo.
Dk Mwakyembe alisema si kwamba serikali inapingana na uamuzi wa
Mahakama Kuu ila kinachofanyika ni utaratibu wa kawaida ambao
utaiwezesha Serikali kuwa na uamuzi kutoka katika chombo cha juu kabisa
cha Mahakama nchini.
Alisema uamuzi huo hautaweza kutenguliwa na mtu au chombo chochote na
kuongeza kuwa ukibaki uamuzi huo pekee katika ngazi hiyo ya Mahakama
inaweza ikatokea siku nyingine Jaji mwingine akatoa uamuzi tofauti na
huo.
Awali, Taasisi ya Msichana Initiative ilifungua kesi ya kikatiba
katika Mahakama Kuu ya Tanzania, shauri namba 5 la mwaka 2016 dhidi ya
Mwanasheria Mkuu wa Serikali ikihoji uhalali wa kikatiba wa kifungu cha
13 na 17 cha Sheria ya Ndoa ya Mwaka 1971 unaoidhinisha mtoto wa kike wa
miaka 14 na 15, kuolewa kwa idhini ya mzazi au Mahakama.
Mahakama Kuu iliamuru vifungu hivyo vifutwe kwa kuwa viko kinyume cha
Katiba ambayo inatamka kuwa umri wa mtoto ni hadi miaka 18 na kuolewa
katika umri huo ni kuvunja sheria mama (Katiba).
chanzo;habarileo.
Comments