MKUU wa Operesheni katika Kanda Maalumu ya Polisi Dar es Salaam,
Lucas Mkondya amewataka wananchi wa mkoa huo kutoshiriki maandamano ya
aina yoyote ambayo yako kinyume na sheria, kwani jeshi hilo limejipanga
kudhibiti maandamano yoyote.
Alitoa kauli hiyo jana wakati wa ziara ya Mkuu wa Mkoa wa Dar es
Salaam, Paul Makonda katika Makao Mkuu ya Kikosi cha Kutuliza Ghasia
(FFU) cha Mkoa kilichopo Ukonga katika Manispaa ya Ilala.
Kauli hiyo ya Mkondya imekuja baada ya Makonda kuwataka askari hao
kuhakikisha wanapambana na vurugu zozote zinazoashiria uvunjifu wa amani
ikiwemo maandamano yanayotarajiwa kufanyika ya Ukuta yaliyoandaliwa na
Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) ili kuhakikisha mkoa unabaki
kuwa na amani.
Alisema kumekuwa na maagizo yanayotolewa na wanasiasa kuhusu uwepo wa
maandamano, lakini ni vyema wananchi wakapuuza na kuepuka kujihusisha
na maandamano hayo kwani askari hao wamejipanga kudhibiti.
"Tumejiandaa vizuri tumeyasikia maandamano ya Ukuta niwatahadharishe
tu wananchi msidanganywe mkakubali kufanya maandamano tumejipanga,
tutawashughulikia hatuna mchezo ni lazima wananchi mtii sheria bila
kushurutishwa," alisema Mkondya.
Kwa upande wake, Makonda ametaka askari hao kufanya kazi kwa weledi
na kuhakikisha wanapambana na wavunja sheria wote bila kumuonea mtu na
kufanya mkoa huo kuendelea kubaki katika hali ya amani na utulivu.
“Hatuko tayari kuona amani ya Mkoa wa Dar es Salaam inavunjika kwa
sababu ya watu wanaokataa kutii sheria ni lazima washurutishwe bila
kumuonea mtu ili amani ya Mkoa huu ibaki kuwa ya mfano katika mikoa
mingine,” alisema Makonda.
Pia Makonda amewaahidi askari hao kuwa, atafanya mazungumzo na
viongozi wa juu ili kuwepo utaratibu wa asilimia 20 ya mapato
yanayokusanywa na Polisi yarudishwe kwao ili yatumike kuboresha mahitaji
mbalimbali ya askari.
“Ninyi ni watu muhimu tunaowategemea kulinda amani yetu na mali zetu,
mmekubali kula kiapo cha kifo kwa ajili yetu ni lazima tuhakikishe
tunaboresha mahitaji yenu na kutatua changamoto zenu,” alisema Makonda.
Aidha, Makonda pia amewaahidi kupeleka gari la kubebea wagonjwa
katika hospitali ya kikosi hicho lengo likiwa ni kuondoa adha
wanayokutana nayo wakati wanapotaka kusafirisha wagonjwa walio katika
hali mbaya.
chanzo;habarileo.
Comments