WAZIRI wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, William Lukuvi
amefuta umiliki wa ardhi yenye ukubwa wa ekari zaidi ya 2,188 mkoani
Kagera iliyokuwa ikimilikiwa na mwekezaji mwenye Kampuni ya Rockshield
Quality Food Processors Ltd ya Uingereza baada ya kuonekana kutofuata
taratibu za umiliki kama sheria ya ardhi inavyotaka.
“Kwa mamlaka niliyopewa kutokana na umiliki wako kutofuata sheria na
taratibu za ardhi, nafuta umiliki wa ardhi hiyo, kwa hiyo nakuagiza
Kamishina Msaidizi wa Kanda ya Ziwa, Joseph Shewiyo ndani ya wiki moja
ardhi hiyo aliyokuwa anamiliki George Rogas kurudishwa kama ilivyokuwa
zamani. Pia wewe mwekezaji ukitaka kuwekeza tunakukaribisha na ufuate
sheria,” ameagiza Lukuvi.
Uamuzi huo umekuja baada ya wananchi wa kata ya Nyanga katika
Manispaa ya Bukoba kulalamikia kuvamiwa na mwekezaji huyo raia wa
Uingereza, George Rogas anayedaiwa kuwanyanyasa na kuwapiga, kisha
kuvamia maeneo yao ya makazi tofauti na ardhi ya ekari tano
alizomilikishwa kihalali na manispaa hiyo.
Mmoja wa wananchi wa eneo hilo, Deodatus Balile alisema kata hiyo
yenye vijiji vitatu ina ekari 1,863, lakini jambo la kushangaza
mwekezaji huyo anadaiwa amejimilikisha ekari 2,119 ambazo ni mali ya
wananchi wa kata hiyo.
chanzo;mpekuziblog.
Comments