Mradi kukarabati vyuo vya ualimu wazinduliwa.

SERIKALI kupitia Wizara ya Elimu, Sayansi, Teknolojia na Mafunzo ya Ufundi, imezindua rasmi mradi mkubwa wa ukarabati na ujenzi wa vyuo vya ualimu nchini, lengo likiwa kuwajengea wanachuo na wakufunzi mazingira mazuri ya kufundishia na kujifunzia.

Akizungumza katika uzinduzi huo uliofanyika katika Chuo cha Ualimu Kitangali mkoani Mtwara mwishoni mwa wiki, Katibu Mkuu Wizara ya Elimu, Sayansi, Teknolojia na Mafunzo ya Ufundi, Maimuna Tarishi alisema gharama ya ujenzi katika vyuo vya ualimu vinne itakuwa Sh 36,475,000,000.

Alivitaja vyuo hivyo kuwa ni Kitangali iliyopo Newala, Mpuguso iliyopo Rungwe, Ndala iliyopo Nzega na Chuo cha Ualimu Shinyanga kilichopo Manispaa ya Shinyanga.

“Suala la kutoa elimu bora lina mambo mengi ndani yake, ili kutimiza dhamira hii inahitajika kuwa na walimu wa kutosha, vitendea kazi, mitaala, vitabu na uboreshaji wa miundombinu, jambo ambalo limeanza kufanyiwa kazi katika mwaka huu wa fedha,” alisema Tarishi.

Aidha, alisema gharama za ujenzi wa miundombinu mipya katika chuo cha Kitangali ni shilingi bilioni nane na kwamba kuanza kwa ujenzi wa chuo hicho ni kuashiria kuanza pia kwa ukarabati na ujenzi katika vyuo vingine vilivyopo katika mpango huu wa awamu ya kwanza, kwa lengo la kuhakikisha mazingira bora ya kufundishia na kujifunzia.

“Shilingi bilioni nane zitakazotumika katika ujenzi wa hapa Kitangali zinapaswa kuleta manufaa kwa wananchi wanaozunguka chuo hichi, hivyo nawaasa wakandarasi kuwatumia wananchi wa maeneo yanayozunguka chuo,” alisisitiza Katibu Mkuu.

Akizungumzia ujenzi wa Chuo cha Ualimu Kitangali, Katibu Mkuu alisema baada ya kutembelea chuo hicho na kuiona miundombinu yake jinsi ilivyochaa alijiridhisha kwamba haiwezi kukarabatiwa na kukubaliana ufanyike ujenzi wa miundombinu mipya.

Naye Ofisa kutoka Idara ya Elimu ya Ualimu, Fredrick Shuma alisema mradi wa ujenzi na ukarabati wa vyuo vya ualimu vinne unafadhiliwa na Serikali ya Tanzania kwa kushirikiana na Serikali ya Canada kupitia Shirika la Mambo ya Nchi za Nje na Maendeleo ya Biashara ambayo inachangia Sh bil 28. 27 na Serikali ya Tanzania inachangia kiasi cha Sh bil 8.2.

“Ujenzi na ukarabati wa vyuo hivyo vinne ukikamilika utaongeza udahili wa wanachuo kutoka 1,643 hadi kufikia 2,950 hivyo kuongeza wanachuo 1,318 katika vyuo hivyo vinne,” alifafanua ofisa huyo wa Idara ya Elimu ya Ualimu.

chanzo;habarileo.

Comments