WOSIA ulioachwa na Rais mstaafu wa Awamu ya Pili wa Zanzibar,
Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi na Makamu wa Rais wa Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania, Aboud Jumbe Mwinyi umezidisha simanzi katika kifo
chake kilichotokea Dar es Salaam jana.
Wakati wa uhai wake, Jumbe (96) aliagiza maziko yake kuwa ya kawaida
kwa mujibu wa misingi ya dini ya Kiislamu, ingawa familia yake imesema
hatua hiyo haiwazuii viongozi wa serikali kuhudhuria shughuli nzima za
mazishi yake.
Akizungumza na waandishi wa habari nyumbani kwa Jumbe, Mjimwema
Kigamboni, Dar es Salaam jana, msemaji wa familia, mtoto wa marehemu,
Mustafa Aboud Jumbe pamoja na kueleza kuwa marehemu atazikwa katika
makaburi ya Migombani, mjini Unguja Zanzibar leo, alisema sharti
lililowekwa na kiongozi huyo la maziko yake kuwa ya kawaida na ya
misingi ya dini, litazingatiwa kama alivyoagiza wakati wa uhai wake.
Mustafa, ambaye ni Katibu Mkuu wa Wizara ya Ujenzi ya Zanzibar,
alikuwa akizungumza juu ya kutokea kwa kifo hicho, ambacho alisema
kimesababishwa na maradhi ya utu uzima.
“Marehemu atazikwa kwa maziko ya kawaida ya Kiislamu kwa mujibu wa
maagizo yake aliyoyaacha, na sisi tunayaheshimu hayo maagizo. “Lakini
haizuii viongozi wa Serikali kushiriki shughuli hii. Unajua mzee alikuwa
mtu wa dini sana, kwa hiyo mwenyewe alituusia hivyo atakapokufa basi
azikwe maziko ya Kiislamu kwa mujibu wa dini yetu,” alisema Mustafa
ambaye ni mtoto wa tano wa Jumbe.
Alisema mwili wake utasafirishwa leo asubuhi kuelekea Zanzibar kabla
ya kupelekwa katika Msikiti wa Mwembeshauri mjini Unguja saa sita
adhuhuri kwa ajili ya kuuswalia na kisha kuzikwa katika makaburi ya
Migombani mjini humo.
Rais Magufuli atuma salamu Katika tukio jingine, Rais John Magufuli
amemtumia salamu za rambirambi Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza
la Mapinduzi, Dk Ali Mohamed Shein kutokana na kifo hicho.
Katika salamu zake jana, Rais Magufuli alisema “Nimeshitushwa sana na
kifo cha Mzee wetu Mheshimiwa Aboud Jumbe, kwa hakika Tanzania
imepoteza mtu muhimu ambaye katika kipindi cha uongozi wake, alitoa
mchango mkubwa wa kuipigania na kuijenga Tanzania tunayoiona leo.”
Jumbe alikuwa Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi
na pia alikuwa Makamu wa Kwanza wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania kuanzia Mwaka 1972 hadi 1984.
Rais Magufuli alisema Taifa limempoteza mtu muhimu ambaye alijitoa
kupigania uhuru, umoja, haki na maendeleo ya wananchi wa Zanzibar na
Tanzania kwa ujumla katika kipindi kigumu ambacho Taifa lilikipitia.
“Kupitia kwako Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi,
Dk Ali Mohamed Shein napenda kuwapa pole familia ya marehemu, ndugu,
jamaa na marafiki wote, wananchi wa Zanzibar na Watanzania wote kwa
ujumla kwa kufikwa na msiba huu mkubwa,” alisema Rais Magufuli Kwa
upande wake Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais anayeshughulikia
Muungano na Mazingira, January Makamba akizungumza na gazeti hili jana
alisema wamepokea taarifa ya msiba huo kwa masikitiko na tayari
maandalizi ya mazishi ya kiongozi huyo yanafanyika baina ya serikali na
familia yake.
“Tumepokea taarifa za kifo kwa masikitiko makubwa kwa kuondokewa na
kiongozi wetu, kichama na serikali, tayari Makamu wa Rais, Samia Suluhu
Hassan ameshaenda Zanzibar kwa ajili ya maandalizi hayo. “Mwili wa
marehemu utasafirishwa kesho (leo) kwenda Zanzibar na baadaye maziko
yatafanyika saa saba mchana na yataongozwa na viongozi mbalimbali wa
chama na serikali.”
Jumbe atakumbukwa kwa mchango wake mkubwa wa kuiongoza Serikali ya
Mapinduzi ya Zanzibar akichukua nafasi ya aliyekuwa Rais wa nchi hiyo,
Abeid Amaan Karume aliyefariki mwaka 1972.
Enzi za uhai wake akiwa Rais wa Serikali ya mapinduzi Zanzibar
alishirikiana na Rais wa wakati huo wa Tanzania na Mwenyekiti wa Chama
cha TANU, Julius Nyerere kuanzisha Chama Cha Mapinduzi (CCM) kwa
kuunganisha vyama vya TANU na ASP na kuunda chama kimoja.
Kwa upande wake, Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar imeeleza
kusikitishwa na kifo hicho cha Jumbe. Taarifa iliyotolewa na Waziri wa
Nchi Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais, Mohamed Aboud mjini Zanzibar jana
ilisema Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar imesikitishwa na kifo hicho.
“Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar imesikitishwa na kifo cha Alhaji
Aboud Jumbe ambaye alikuwa Rais wa Zanzibar kwa muda wa miaka 13 huku
mchango wake mkubwa katika kukuza na kuimarisha demokrasia ukibakia
kielelezo kwa wananchi wa Zanzibar na Tanzania kwa ujumla,” ilisema
taarifa hiyo.
Kwa mujibu wa taarifa za kutoka kwa familia ya Jumbe, maziko yake
yanatarajiwa kufanyika leo mchana nyumbani kwake Migombani nje kidogo ya
mji wa Zanzibar, eneo ambalo watoto wake watatu wamezikwa hapo.
Historia yake kisiasa.
Jumbe alishika madaraka ya kuongoza Zanzibar katika mwaka 1972 baada
ya kuuawa kwa Abeid Amaan Karume ambapo Baraza la Mapinduzi kwa kauli
moja lilimchagua kushika wadhifa huo wa Rais wa Zanzibar.
Kutokana na kuchafuka kwa hali ya kisiasa Zanzibar katika mwaka 1984,
Jumbe alilazimika kujiuzulu pamoja na viongozi wengine akiwemo Waziri
Kiongozi Ramadhan Haji Faki na hivyo kupoteza nyadhifa zote, ikiwemo
Makamu wa Rais wa Muungano na Makamu Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi
(CCM).
Jumbe atakumbukwa kwa mambo mengi akiwa ni mmoja ya viongozi
walioshirikiana na Mwalimu Nyerere kuzaliwa kwa CCM mwaka 1977 katika
Uwanja wa Amaan Zanzibar.
Kabla ya kuzaliwa kwa CCM, Jumbe alikuwa Rais wa Chama cha ASP ambapo
ushawishi wake mkubwa ndiyo uliosababisha kuunganishwa kwa vyama hivyo
na kuzaliwa kwa CCM, ikiwa ni moja ya juhudi za kuimarisha Muungano wa
Tanganyika na Zanzibar.
Katika kuimarisha demokrasia na sauti za wananchi kusikika, Jumbe
alianzisha chombo cha kutunga sheria ambacho alikiita Baraza la
Wawakilishi. Baraza la Wawakilishi liliasisiwa katika mwaka 1979 kwa
kuanzia viongozi kutoka katika Wilaya za Unguja na Pemba kwa
kuzishirikisha jumuiya za chama ikiwemo Umoja wa Vijana, Wazazi,
Ushirika na Umoja wa Wanawake (UWT).
Huo ndiyo mchango mkubwa wa Jumbe katika kuanzisha chombo cha Baraza
la Wawakilishi ambalo aliliita ngome ya wananchi katika kusikiliza maoni
yao.
CCM yasikitishwa
Wakati huo huo, CCM Zanzibar imeeleza kusikitishwa na kifo cha
Jumbe.Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Naibu Katibu Mkuu wa CCM
Zanzibar Vuai Ali Vuai, mchango wa Jumbe katika CCM hautasahaulika.
“Chama Cha Mapinduzi kinatoa masikitiko yake makubwa kutokana na
msiba mkubwa wa aliyekuwa Makamu Mwenyekiti wake wa kwanza Jumbe.
Mchango wake hautasahaulika katika Chama Cha Mapinduzi,” alisema.
Alisema Jumbe alihakikisha kinazaliwa chama kipya kitakachokuwa na
nguvu pamoja na sura ya Muungano kwa ajili ya faida ya wananchi wa
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Alisema tangu kuzaliwa kwa chama hicho,
kimeendelea kupata mafanikio makubwa ikiwemo kushinda katika chaguzi
zote kuanzia za mfumo wa chama kimoja hadi vyama vingi.
Aidha chama hicho kimeendelea kuwa imara bila ya kuyumba na kuendelea
kushika hatamu ya kuongoza dola katika kipindi chote kuanzia mwaka 1977
hadi leo.
“Mafanikio yote ya Chama Cha Mapinduzi hatuna budi kukumbuka juhudi
zilizofanywa na hayati Jumbe kwa sababu ndiye aliyekiunganisha chama
hicho kutoka ASP na TANU na kuzaliwa CCM,” alisema Vuai.
chanzo;habarileo.
Comments