Majaliwa aagiza Temeke, Kigamboni wagawane mali.

WAZIRI Mkuu, Kassim Majaliwa amewataka viongozi wa wilaya za Temeke na Kigamboni iliyozaliwa kutoka ubavuni mwa Temeke, kuanza kugawana mali badala ya watumishi.

Agizo hilo limekuja baada ya Kigamboni kupata Mkuu mpya wa Wilaya ambaye ni Hashim Mgandilwa.

Waziri Mkuu alisema hatua hiyo itasaidia kuondoa migogoro baina ya pande hizo kwani watagawana mali wakiwa wamoja. Akizungumza na watumishi wa Manispaa ya Temeke mkoani Dar es Salaam hivi karibuni, Majaliwa alisema kuanza kugawa watumishi kabla ya mali kumesababisha maeneo mengi kuwa na ugomvi usiokoma, akitolea mfano Mbinga na Nyasa, mkoani Ruvuma.

Alisema wanapogawana sasa watafanya kwa haki, lakini wakishagawa watumishi watakuwa wanavutia kwao huku ugomvi ukihamia hadi katika Baraza la Madiwani watakaokuwa wanatumwa na watendaji.

Alisema pia Meya wa Temeke kama kata yake itaangukia Temeke atabaki kuwa meya wa huko lakini kama ataangukia Kigamboni, italazimu kufanyika upya kwa uchaguzi wa meya. Pia amewahimiza watendaji Manispaa ya Temeke kuimarisha makazi mapya kwa kuhamasisha ujenzi wa majengo ya kisasa tofauti na mengi yaliyojengwa kiholela.

Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda alisema katika kuhakikisha wananchi wanapata huduma bora za afya, amezungumza na Balozi wa Japan nchini na kukubali kujenga sehemu za kutoa huduma ya dharura kwa haraka.

Alisema kwa kuanzia watajenga katika Manispaa ya Temeke na kufuatia katika wilaya nyingine za Ilala na Kinondoni kutokana na takwimu zikieleza watu nusu ya wagonjwa 6,000 wa kila siku wanahitaji huduma ya haraka kila siku katika jiji hilo.

chanzo;habarileo

Comments