RAIS John Magufuli amemteua na kumwapisha Dk Modestus Francis
Kipilimba kuwa Mkurugenzi Mkuu wa Idara ya Usalama wa Taifa (TISS).
Dk Kipilimba aliapishwa Ikulu Dar es Salaam jana mchana, saa chache baada ya uteuzi wake uliotangazwa asubuhi.
Kwa mujibu wa taarifa ya Ikulu, baada ya kuapishwa kuwa Mkurugenzi
Mkuu wa Idara ya Usalama wa Taifa, Dk Kipilimba alikula kiapo cha
Uadilifu kwa Viongozi wa Umma kilichoongozwa na Kamishna wa Maadili,
Jaji mstaafu Salome Kaganda.
Kabla ya uteuzi huo, Dk Kipilimba alikuwa Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa
Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa (NIDA), na amechukua nafasi iliyoachwa
wazi na Rashid Othman ambaye amestaafu utumishi wa umma mwishoni mwa
wiki iliyopita.
Aidha, Rais Magufuli alimteua Robert Msalika Makungu kuwa Naibu Mkurugenzi Mkuu wa Idara ya Usalama wa Taifa Tanzania Bara.
Kabla ya uteuzi huo, Makungu alikuwa Ofisa Ubalozi katika Ubalozi wa
Tanzania nchini Ethiopia. Pia Rais Magufuli amemteua aliyekuwa Kaimu
Mkurugenzi Mkuu wa Idara ya Usalama wa Taifa, George Madafa kuwa Balozi
na nchi atakayopangiwa itatajwa baadaye.
Taarifa ya Ikulu ilieleza kuwa wakurugenzi na naibu wakurugenzi wa Idara ya Usalama wa Taifa waliopo wanaendelea na nafasi zao.
chanzo;habarileo.
Comments