Rais
wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli amesema
serikali yake haitagawa chakula cha bure kwa wananchi wanaopatwa na
tatizo la njaa pasipo kuwa na sababu za msingi na badala yake amewataka
watanzania wajikite kufanya kazi kwa juhudi na maarifa ikiwa ni pamoja
na kuzalisha chakula cha kutosha.
Rais Magufuli amesema hayo jana tarehe 31 Julai, 2016 wakati
akihutubia mikutano ya hadhara na kuzungumza na wananchi waliosimamisha
msafara wake akiwa njiani kutoka Mkoani Tabora kuelekea Shinyanga na
baadaye Geita anakoendelea na ziara yake.
Pamoja na kuwahimiza wananchi kuzalisha chakula cha kutosha ili kuondokana na njaa Rais Magufuli amesema serikali yake itajikita kuhakikisha inashughulikia tatizo la uhaba wa maji, ujenzi wa miundombinu hususani barabara na reli, kuimarisha huduma za matibabu, elimu na kutengeneza ajira.
Akiwa Isaka Mkoani Shinyanga Rais Magufuli amesema serikali haitalipa
fidia kwa wananchi waliopatwa na maafa ya mafuriko yaliyobomoa nyumba
zao mwezi Machi mwaka 2015 na badala yake itajielekeza kutatua tatizo
kubwa la uhaba wa maji katika mji huo ambao una makutano ya reli ya kati
ya kutoka Dar es Salaam kwenda nchi za Burundi na Rwanda.
Katika Mji wa Kagongwa Rais Magufuli amepokea kilio cha wananchi
dhidi ya vitendo vya ujambazi na ametoa siku tano kwa Kamanda wa Polisi
wa Mkoa wa Shinyanga kuhakikisha watu wanaojihusisha na ujambazi
wanakamatwa na kufikishwa katika vyombo vya sheria.
Mjini Kahama, Dkt. Magufuli ameiagiza Wizara ya Nishati na Madini
kushirikiana na Mbunge wa Kahama Mhe. Jumanne Kishimba kukokotoa
mahesabu vizuri na kubaini kodi ambayo Serikali inastahili kulipwa baada
ya Mbunge huyo kudai kuna kiasi kikubwa cha kodi hakijakusanywa kama
ambavyo sheria inaelekeza.
Aidha, Rais Magufuli amesema serikali itahakikisha wawekezaji
wanaochimba madini wanaacha kusafirisha mchanga wenye madini kwa lengo
la kwenda kuchakata nje ya nchi na badala yake ametaka uchakataji huo
ufanyike hapa hapa nchini.
Dkt. Magufuli amezungumza na wananchi vijiji vya Segese na Bukoli na
kuwahakikishia kuwa Barabara ya Kahama, Segese, Kakola hadi Geita yenye
urefu wa kilometa 146 itajengwa kwa kiwango cha lami kama alivyoahidi.
Mjini Geita, Rais Magufuli amepokea kilio cha wananchi wanaodai
kuwekewa zuio la kutumia mawe yenye mabaki ya madini ya dhahabu
(Magwangala) kwa lengo la kusaga na kuchenjua ili kupata dhahabu, na
ametoa wiki tatu kwa Wizara ya Nishati na Madini kwa kushirikiana na
Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC) kufanya
tathimini na kuwaruhusu wachimbaji wadogo kutumia Magwangala.
Rais Magufuli pia ameiagiza Bodi ya Pamba hapa nchini kuhamisha ofisi
zake zilizopo Jijini Dar es salaam na kuzileta katika Mikoa ya kanda ya
ziwa ambako uzalishaji wa zao la pamba unafanyika.
Dkt. Magufuli amewaonya viongozi na watendaji wa bodi hiyo dhidi ya
vitendo vya usambazaji wa mbegu za pamba zisizoota na amesema ikitokea
tena watachukuliwa hatua.
Leo tarehe 01 Agosti, 2016 Rais Magufuli ambaye ameongozana na
Mkewe Mama Janeth Magufuli anatarajia kukamilisha ziara yake ya siku nne
katika Mikoa ya Singida, Tabora, Shinyanga na Geita.
chanzo;ubuyublog.
Comments