WATU bilioni 3.9 duniani watakuwa na tatizo kubwa la maji ifikapo mwaka 2050 na hivyo kusababisha uwezekano wa kusambaa kwa magonjwa yanayosababishwa na matumizi ya majitaka.
Hayo yalielezwa na Mtaalamu wa Ikolojia ya Bakteria kutoka Chuo Kikuu cha Brighton, Profesa Huw Taylor wakati akizungumzia Mradi wa Shirika la Umoja la Mataifa la Elimu, Sayansi na Utamaduni (Unesco) wa kuweka mfumo mpya wa udhibiti na Menejimenti ya Majitaka (GWPP).
Profesa Taylor alisema kutokana na ukweli huo, kwa sasa Unesco kwa kushirikiana na Chuo Kikuu cha Michigan kinatafuta na kueleza kwa wadau wake suala la maji na namna ya kuhakikisha kwamba kila mtu anakuwa na maji ya kutosha na salama.
Alisema mpango wa dunia wa maendeleo endelevu hauwezi kufanikiwa kama tishio la majitaka litaendelea kuwapo na lazima binadamu aendelee kujipanga kuhakikisha kwamba anatawala mazingira ya maji na ana mfumo bora wa udhibiti wa majitaka na madhara yake.
Unesco mwishoni mwa wiki jijini Dar es Salaam iliendesha kongamano lililoshirikisha wataalamu takribani 100 kutoka nyanja mbalimbali kuzungumzia mradi huo wa GWPP.
Kongamano hilo lililofunguliwa na Katibu Mkuu wa Wizara ya Maji na Umwagiliaji, Mbogo Futakamba ambaye hotuba yake ilisomwa kwa niaba na Mkurugenzi Msaidizi katika wizara hiyo, Dk George Lugomelo, lililenga kujadili kwa kina matatizo ya bakteria wanaosababisha magonjwa katika maji na madhara yake.
Akihutubia, Katibu Mkuu huyo aliwataka wataalamu kuhakikisha wanaelewa dhana ya GWPP, kuisaidia na kuhakikisha kwamba inapata majibu sahihi ili kuiwezesha kuwa na mfumo unaoeleweka wa udhibiti wa maji machafu na menejimenti yake.
Mradi huo wa Unesco ambao unajulikana kama Global Water Pathogen Project (GWPP) utamalizika mwakani kwa kutengenezwa kitabu ambacho kitakuwa kimefanya marekebisho makubwa ya kitabu kilichotungwa miaka 40 iliyoipita ambayo yaliweka alama teule ya mwisho ya usalama wa maji na mejimenti ya maji taka.
Katibu Mkuu alisema ingawa asilimia 93 ya Watanznaia ina vyoo ni asilimia 24 tu ndio wenye vyoo bora. Alisema kutokana na watu kuwa na mazoea ya kutumia vichaka na kwenye maji hatari ya kupata magonjwa yanayosababishwa na matumizi ya maji machafu kama kuhara na kipindupindu ni kubwa.
chanzo;hgabrileo.
Comments