Shirika la Umeme Zanzibar (ZECO) kwa Kushirikiana na Kampuni ya Simu ya Zantel Wamerudisha Huduma ya Ezypesa kwa Wanunuzi wa Umeme kwa Njia ya Simu.

Kampuni ya simu ya ZANTEL kwa kushirikiana na Shirika la Umeme Zanzibar, ZECO, leo wamezindua upya huduma ya kununua umeme kwa kutumia huduma ya Ezypesa visiwani Zanzibar.
Huduma hiyo inayojulikana kama TUKUZA, ilisitishwa miezi michache iliyopita kutokana na hitilafu za kiufundi, na sasa imeboreshwa zaidi kuweza kuhudumia wateja wengi zaidi na kwa ufanisi mkubwa zaidi.
Akizungumza katika hafla fupi ya uzinduzi wa huduma hiyo, Afsa Mtendaji Mkuu wa Zantel, Bw. Benoit Janin, alisema Zantel itaendelea kuwa msitari wa mbele kutoa huduma zitakazorahisisha maisha ya wateja wake.
'Toka kampuni ya Millicom ilipoingia, tuliahidi kuboresha huduma zetu, lakini pia kuhakiskisha huduma hii ya TUKUZA inaanza kufanya kazi kwa ufanisi mkubwa, na leo tuna furaha kuizindua huduma hii tena, na kwa uwekezaji tuliofanya tunaamini hakutakuwepo na hitilafu tena’ alisema Janin.
Maboresho hayo katika huduma ya TUKUZA yanatarajia kuwapa faida mbalimbali wateja wa ZECO na Zantel ikiwemo kuongezeka kwa spidi ya mfumo, pamoja na kumaliza kabisa tatizo la foleni katika vituo vya ZECO.
Naye Mkurugenzi Mtendaji wa ZECO, Bw Hassan Ali Mbarouk, alisema kuboreshwa kwa huduma hiyo ni hatua muhimu ya kuwawezesha wateja wa visiwani humu kupata huduma bora na pia kuongeza kipato kwa mawakala wa Ezypesa.
'Kupitia simu zao za mikononi wateja wetu wataweza kutumia huduma ya Ezypesa kununua umeme na kulipia bili zao, mahali popote na kwa muda wowote na hivyo basi kupunguza gharama za kwenda kwenye vituo vya ZECO kununua umeme’ alisema Mbarouk.

chanzo;zanzinews.
Comments