MTUHUMIWA wa ujambazi Msafiri Suleiman maarufu kama Juma Msukuma ameuawa wakati akijaribu kuwatoroka Polisi.
Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Mwanza, Ahmed Msangi alisema jana kuwa
tukio hilo lilitokea Julai 28 mwaka huu majira ya saa 10.30 jioni katika
eneo la Igoma kata ya Igoma jijini Mwanza.
Kamanda Msangi alisema mtuhumiwa siku hiyo alikuwa amekamatwa na
Polisi akituhumiwa kufanya matukio ya unyang’anyi wa kutumia silaha
akishirikiana na wenzake watatu.
Aliwataja watu hao aliokuwa akishirikiana nao ambao kwa sasa
wamekamatwa na polisi kuwa ni Jackson Magesa ( Nyakibimbi), Samwel Mwita
na Boniphace Nyamhanga.
Kamanda alisema baada ya mahojiano na polisi mtuhumiwa alikiri
kuhusika na uhalifu na akakubali kwenda kuwaonesha askari sehemu
aliyoficha silaha maeneo ya Buhongwa mlimani.
Alisema walipofika eneo husika aliwaonesha mkasi mkubwa wa kukatia
vyuma na kipande cha nondo, huku akiwathibitishia kuwa silaha alikuwa
ameichimbia ardhini katika eneo hilo.
“Wakati askari wakiwa kwenye harakati za kufukua ili waichukue silaha
hiyo, mtuhumiwa alitumia mwanya huo kuanza kukimbia huku akiwa na pingu
mkononi, askari walifyatua hewani risasi tatu, lakini mtuhumiwa hakutii
amri hiyo ndipo alipopigwa risasi mguuni na kufanikiwa kukamatwa”,
alifafanua.
Alisema alifariki dunia akiwa njiani kupelekwa hospitali.
“ Watuhumiwa aliokuwa akishirikiana nao tumewakamata na tumewakuta
wakiwa na bunduki aina ya Rifle Mark 4 ikiwa na risasi nne, ikiwa na
kitako cha bunduki waliyopora, nyundo moja na vipande vitatu vya nondo”,
alisema.
“ Watuhumiwa hao tunawashikilia kwa matukio ya unyang’anyi Nyashishi,
Buhongwa, Bulale, Nyambichi na Mwananchi ambapo walipora silaha toka
kwa mlinzi wa Kampuni ya Paroma Patrol Security Service”, aliongeza.
chanzo;habarileo.
Comments