RAIS John Magufuli amemteua Dk Samuel Nyantahe kuwa Mwenyekiti wa Bodi ya Shirika la Maendeleo la Taifa (NDC) kuchukua nafasi iliyoachwa wazi na Dk Christant Mzindakaya ambaye amejiuzulu wadhifa huo.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Katibu Mkuu Kiongozi, Balozi John Kijazi, Ikulu jana mjini Dodoma, uteuzi huo umeanza Julai 20, mwaka huu.
Taarifa hiyo inasema kabla ya uteuzi huo, Dk Nyantahe alikuwa Mwenyekiti wa Shirikisho la Wenye Viwanda Tanzania (CTI).
Wiki iliyopita, Mzindakaya (76) aliwaambia waandishi wa habari kuwa amemuandikia barua Rais Magufuli kumuomba amruhusu kupumzika na kuacha nafasi hiyo kabla ya muda wake kuisha.
Alisema sababu ya kuomba kuachia nafasi hiyo aliyotakiwa kuishika mpaka Julai mwakani ni utu uzima ulioambatana na mwili kuchoka.
Mzindakaya aliyekuwa mbunge kwa miaka 44, alisema kwa sasa ni mzee hivyo anahitaji kupumzika kwa hiyo anaona ni vyema kuachia nafasi hiyo kwa kuwa inahitaji kusafiri ndani na nje ya nchi, hivyo inamhitaji mtu mwenye nguvu. Alisema anabaki kuwa mshauri atakapohitajika kufanya hivyo.
chanzo;habarileo.
Comments