SERIKALI itahakikisha inalipa deni la Taasisi ya Saratani ya Ocean
Road (ORCI) katika Bohari Kuu ya Dawa (MSD) ili wagonjwa wapate dawa za
saratani kwa gharama nafuu.
Kauli hiyo imetolewa na Makamu wa Rais, Samia Suluhu Hassan wakati
alipotembelea taasisi hiyo pamoja na kumtembelea na kumjulia hali Katibu
Mtendaji wa Kamisheni ya Utalii ya Zanzibar, Saleh Ramadhani Feruzi
ambaye anapatiwa matibabu hospitalini hapo.
Alisema kwamba serikali itahakikisha inalipa deni hilo hata kama si
lote ili kuwaondolea adha wagonjwa wa saratani ya kununua dawa katika
maduka binafsi ambako ni ghali.
Akizungumza na baadhi ya wagonjwa ambao walimlalamikia gharama kubwa
za dawa za matibabu aliahidi kuwa serikali itafanya jitihada zote ili
wananchi hao wapate dawa hizo kwa gharama nafuu. “...Tutajitahidi
serikali ilipe deni la MSD hata kama si lote lakini tupunguze ili
wagonjwa wapate dawa kwa unafuu, kuliko kwenda kununua katika maduka
binafsi basi wazipate hapa hospitali kwa bei ya unafuu,” alisema Samia.
Aidha, Samia alisema serikali itanunua mashine mbili za kisasa za
mionzi kwa ajili ya taasisi hiyo ambazo zitasaidia utoaji wa matibabu
kwa wagonjwa wanaofuata huduma katika taasisi hiyo.
Alisisitiza kuwa mkakati wa serikali uliopo unalenga kuhakikisha kuwa
hali ya utoaji wa huduma za afya na dawa kote nchini unaimarika ili
wananchi waweze kupata huduma hizo kwa ubora unaotakiwa.
Katika hatua nyingine alisema, amejionea tatizo la uhaba wa wahudumu
na pia Mganga Mkuu wa taasisi hiyo amemuambia kuwa wameomba kibali cha
kuajiri wahudumu wa afya 100, ambapo aliahidi kuwa serikali itahakikisha
katika mwaka wa fedha 2016/2017 wahudumu wanapatikana wa kutosha.
Naye Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa taasisi hiyo, Dk Diwani Msemo alisema
serikali imetenga takribani Sh bilioni nane kwa ajili ya kupelekwa MSD
kwa ajili ya vifaa tiba na dawa. Dk Msemo aliongeza kuwa kwa sasa,
wanahudumia wagonjwa 160 kwa siku ambapo huanza kazi saa 12:00 asubuhi
hadi saa 6 au 7:00 usiku.
chanzo;habarileo.
Comments