Zanzibar Yaadhimisha Siku ya Makumbusho Duniani May18.

Waziri wa Habari, Utalili, Utamaduni na Michezo Zanzibar Rashid Ali Juma amewataka  wananchi wa Zanzibar kutumia fursa ya  kutembelea Jengo la Makumbusho  ya Mnazimmoja ili kuelewa historia ya  utamaduni  wao .

Waziri Rashid ameyasema hayo katika Sherehe za ufunguzi wa maonesho ya kudumu ya sanaa katika maadhimisho ya  siku ya makumbusho dunuani yaliyofanyika  Makumbusho ya Mnazi mmoja  Mjini Zanzibar.

Amesema Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar  itaendelea kutoa misaada katika Idara ya Mkumbusho na Mambo ya kale ili isibakie nyuma katika ulimwengu  wa sasa  ambapo dunia imekuwa kama kijiji.

Waziri  wa Habari, Utalii Utamaduni na Michezo  amesema wananchi wanahitaji kutunza kumbukumbu na niwajibu kuyatunza maeneo  hayo yasipoteze haiba yake ya asili.

Katibu Mkuu  wa Wizara ya Habari, Utalili, Utamaduni na Michezo Zanzibar Omar Hassan Omar  amesema jengo la makumbusho ni muhimu na linapaswa kutuzwa  kwani mila, desturi na silka za Zanzibar  zinapotea  kutokana na  kukosekana  uhifadhi mzuri.

Aidha ameahidi  kushirikiana na wafanyakazi  wa Idara  hiyo kwa  kuwapatia mafunzo  ya mara kwa mara ili wawe na uwezo wa kutekeleza kazi  zao  kwa ufanisi zaidi .

Katika Risala yao iliyosomwa na Mkuu wa Divisheni ya Makumbusho Khamis Abdallah,  wafanyakazi hao wamesema  wameamua kuandaa maonyesho hayo ya kudumu ya sanaa ili kutoa mwamko na hamasa kwa jamii juu ya upana wa sanaa hiyo.

Wamesema wanajukumu kubwa la kulinda, kuhifadhi  na kutunza  kumbukumbu za taifa  lakini wamekuwa wakikabiliwa na tatizo la maeneo ya kihistoria kuvamiwa na  wananchi.

“Tunajikuta tunajukumu kubwa kwa Serikali na hata kwa mwenyenzi mungu kuona kuwa rasilimali hizi zanaanza kupotea zikiwa  mikononi mwetu”,alisema Khamiss Abdallah.

Maonyesho hayo yamejumuisha  nyanja zote za maisha ikiwemo  Mavazi, Ususi, Ufinyanzi, Uhunzi, Uchoraji na Ujenzi  ikiwa ni utaratibu mzima wa mfumo wa maisha ya Wazanzibari.
chanzo;zanzinews.

Comments