Msemaji wa jeshi la Nigeria amesema kuwa, wanachama 16 wa kundi la Boko Haram wamejisalimisha kwa vikosi vya serikali wakiwemo viongozi kadhaa wa kundi hilo.
Kanali Sani Usuman amesema kuwa, wanachama hao wa Boko Haram wamejisalimisha kwa jeshi la Nigeria katika Wilaya ya Dure kwenye jimbo la Borno.
Msemaji wa jeshi la Nigeria amesema kuwa, viongozi watatu wa Boko Haram yaani Hamidou Buba, Mussa Buba na Ali Isrissa ni miongoni mwa wanachama wa kundi hilo waliojisalimisha kwa jeshi la Nigeria.
Habari ya kujisalimisha wanachama wa Boko Haram inaripotiwa siku chache tu baada ya jeshi la Nigeria kuanzisha operesheni kabambe katika msitu wa Sambisa inayolenga kuwafurusha wanamgambo hao kutoka katika ngome yao hiyo inayotumika kutoa mafunzo.
Msitu wa Sambisa uko katika jimbo la Borno kaskazini mashariki mwa nchi hiyo ya magharibi mwa Afrika na unahesabiwa kuwa ngome kubwa zaidi ya Boko Haram.
Kundi la Boko Haram lililoanzisha machafuko ya ndani nchini Nigeria mwaka 2009 limeua zaidi ya watu elfu 20 na kulazimisha mamilioni ya wengine kukimbia maeneo ya kaskazini mwa nchi hiyo. Mbali na Nigeria wanamgambo hao sasa wanaendesha harakati zao za kigaidi katika nchi za Chad, Niger, Cameroon na hata Benin.
chanzo;parstoday.
Comments