Umoja wa Afrika umetaka uchaguzi wa marudio nchini Comoro ufanyike kwa usalama.


Umoja wa Afrika umetaka uchaguzi wa marudio katika kisiwa cha Anjouan nchini Comoro ufanyike kwa huru na haki nchi Comoro.
Taarifa iliyotolewa na umoja huo mjini Addis Ababa jana Jumamosi, imetaka uchaguzi wa rais uliopangwa kufanywa tarehe 11 mwezi huu katika baadhi ya maeneo ya nchi hiyo ufanyike kwa usalama na amani. 
Nkosazana Dlamini-Zuma, mkuu wa kamisheni ya umoja huo ameelezea wasiwasi wake kuhusiana na matukio ya nchini Comoro, na ametaka uchaguzi huo wa marudio katika kisiwa cha Anjouan uwe salama na kusisitiza kuwa, Umoja wa Afrika tayari umetuma waangalizi wake nchini humo kuhakikisha zoezi hilo linafanyika katika mazingira ya amani. Wiki iliyopita Mahakama ya Katiba nchini Comoro ilitoa amri ya kurudiwa uchaguzi katika maeneo 13 ya nchi hiyo ya visiwa kutokana na dosari zilizojitokeza katika uchaguzi wa tarehe 10 mwezi uliopita wa Aprili. 
Katika duru ya pili ya uchaguzi huo, Rais Azali Assoumani, mmoja wa makamanda wa zamani wa jeshi la nchi hiyo na aliyewahi kuendesha mapinduzi ya kijeshi nchini humo, aliibuka mshindi na kutangazwa kuwa rais wa Comoro.
chanzo;parstoday

Comments