Rais Beji Caid Essebsi wa Tunisia ametangaza habari ya kutenga serikali yake dola bilioni nne kwa ajili ya kupambana na ugaidi.
Shirika la habari la Ufaransa limemnukuu Rais Essebsi akisema hayo jana mwishoni mwa ziara yake ya siku tatu nchini Qatar na kuwaambia waandishi wa habari kuwa, nchi yake imetenga fedha hizo nyingi kwa ajili ya kupambana na ugaidi licha ya kwamba zingeliweza kutumika kwa ajili ya ustawi wa kiuchumi na uwekezaji nchini mwake.
Amesisitiza kuwa, nchi yake imeweka mfumo maalumu wa ulinzi katika mipaka yake na Libya kwa ajili ya kuzuia magaidi kujipenyeza nchini humo.
Rais wa Tunisia amesema pia kuwa, mipaka hiyo imekuwa na usalama zaidi katika miezi mitano iliyopita tangu mfumo huo wa ulinzi uanze kufanya kazi.
Mwaka jana Tunisia ilishuhudia mashambulio matatu makubwa ya kigaidi yaliyopelekea karibu watu 74 kuuawa wengi wakiwa ni watalii na maafisa usalama wa serikali.
Mashambulizi hayo yalitokea katika jengo la makumbusho la Bardo, Hoteli ya kitaliii katika eneo la Sousse pamoja na shambulizi dhidi ya gadi ya Rais mwaka 2015, ambapo genge la kigaidi la Daesh lilitangaza kuhusika na mashambulio hayo yote.
chanzo;parstoday.
Comments