Taasisi zatakiwa kuanza kutumia alama za EAC.

TAASISI za serikali na idara zake zimeagizwa kuanza kutumia alama za Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC), ambazo ni bendera na wimbo wa jumuiya, ikiwa ni utekelezaji wa mkataba wa uanzishwaji wake.
Akizungumza na wanahabari Dar es Salaam jana, Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano serikalini wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mindi Kasiga, alisema kuanzia sasa matumizi ya alama hizo yanatakiwa yaende sanjari na alama ya taifa ambayo ni bendera ya taifa.
Kasiga alisema, mkataba wa uanzishwaji wa EAC umesisitiza nchi wanachama kushiriki katika jumuiya hiyo na kujenga uzalendo.
Akizungumzia matumizi ya bendera hiyo kwa ngazi za kiutawala, Kasiga alisema kuanzia ngazi ya chini kwenye serikali za mitaa ambako bendera ya taifa inapepea ni lazima na ya jumuiya hiyo ipepee.
“Nitoe mwito kwa taasisi za serikali, wizara, idara, mashirika ya umma, sekta binafsi wote kwa pamoja popote penye bendera ya taifa yaani ya Tanzania, ni lazima pembeni kuwepo na bendera ya EAC,” alisema Kasiga.
Aliongeza, kwenye shughuli rasmi za kiserikali, wimbo wa taifa unapoimbwa ni lazima pia wa EAC uimbwe.
“Hilo ni agizo linaloanza kutekelezwa na nchi zote sita za jumuiya,” alisema. Nchi hizo ni Tanzania, Kenya, Uganda, Burundi, Rwanda na Sudan Kusini.
chanzo;habarileo.

Comments