WIZARA ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa imesema endapo vikosi vya Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) visingekuwapo visiwani Zanzibar na kusimamia hali ya amani na utulivu katika uchaguzi wa marudio, hali ya usalama visiwani humo isingekuwa shwari.
Pia wizara hiyo, imejibu hoja za baadhi ya wabunge hasa wa upinzani na wananchi zinazodai kuwa jeshi hilo lilisambazwa visiwani humo kwa ajili ya kusaidia upande wa CCM ili ushinde, kuwa hazina mashiko, kwani jeshi hilo limekuwapo muda mrefu visiwani kutekeleza majukumu yake.
Hayo yalisemwa bungeni, Dodoma juzi na Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, Dk Hussein Mwinyi wakati akihitimisha hoja za wabunge zilizotolewa wakati mjadala wa kupitisha makadirio ya mapato na matumizi ya fedha kwa mwaka 2016/17 ya wizara hiyo.
“Ndugu zangu naomba nirudie watu wakisikia kwamba jeshi linapelekwa Zanzibar wakati wa uchaguzi, watadhani Zanzibar hakuna jeshi, lakini Zanzibar kuna brigedi, sio platuni wala kombania kuna brigedi,” alisisitiza Dk Mwinyi.
Alisema kuna brigedi ya askari mashuhuri Zanzibar na askari wa vitengo mbalimbali ikiwamo wanamaji na wanaanga, hivyo hoja kwamba jeshi lilipelekwa visiwani humo haina msingi kutokana na ukweli kuwa tayari visiwani humo kuna jeshi.
Alisema jeshi hilo liko Zanzibar kwa madhumuni ya kulinda mipaka ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ambayo Zanzibar iko ndani ya mipaka hiyo. Alikiri kuwa baadhi ya vikosi vya jeshi hilo vilisambazwa katika maeneo nyeti kama uwanja wa ndege kipindi cha uchaguzi kusaidia pindi yanapotokea machafuko.
Alisema tangu jeshi hilo lisambazwe Zanzibar katika harakati za kuhakikisha usalama, limesaidia kwa kiasi kikubwa wananchi kutulia. “Hatuwezi kukataa kuwa mabomu hayakurushwa, kweli yalirushwa hata vyombo vya habari vilisema, kwa hiyo tujiulize kama jeshi lisingekuwepo ile hali ya amani na usalama ingekuwepo mpaka leo?
Alihoji. Akizungumzia tuhuma za baadhi vikosi vilivyopo chini ya Umoja wa Mataifa (UN) kufanya vitendo vya ubakaji, Dk Mwinyi, alisema wizara yake iliunda Tume ya uchunguzi, kuchunguza kama kuna askari wa Tanzania walihusika na tuhuma hizo na wakibainika watachukuliwa hatua.
chanzo;habarileo.
Comments