Serikali kufuta taasisi 200.

SERIKALI iko mbioni kuzifutia usajili taasisi karibu 200 kati ya 5,262 ambazo hazijawasilisha taarifa zake kwa Wakala wa Usajili, Ufilisi na Udhamini (RITA). Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa RITA, Emmy Hudson alisema hayo jana Dar es Salaam na kuweka wazi kuwa taasisi hizo ni zile zilizo chini ya RITA.
Alisema, baada ya Waziri wa Katiba na Sheria, Dk Harrison Mwakyembe kuzitaka taasisi zote zilizoko chini ya RITA kuwasilisha taarifa zao, nyingi zimekuwa kimya mpaka sasa. “Tulitoa tangazo kuwa taasisi zilizopo chini ya RITA ziwasilishe taarifa zake, lakini kuna taasisi karibu 200 hazijaleta ingawa utekelezaji wa agizo hilo ni endelevu,” alisema Hudson.
Alisema, RITA inashindwa kuelewa taasisi hizo ziko hai au zimekufa kwani zinatakiwa kuwasilisha taarifa mbalimbali zinazohusiana na kazi zao. Alisema, hivi karibu RITA itatoa notisi ya siku 30 kwa taasisi hizo kabla ya kuchukua hatua ya kuzifungia kuendelea kutoa huduma.
Aprili mwaka huu, Dk Mwakyembe aliitaka RITA kusitisha usajili wa taasisi za kijamii hadi itakapohakiki zilizosajiliwa chini yake.
chanzo;habarileo.

Comments