Safari ya Rais wa Ufaransa katika Jamhuri ya Afrika ya Kati.

Rais Francois Hollande wa Ufaransa Ijumaa aliitembelea kwa masaa kadhaa Jamhuri ya Afrika ya Kati (CAR)na kukutana na rais wa nchi hiyo Faustin-Archange Touadéra.
Baada ya safar hiyo fupi mjini Bangui, Hollande alielekea katika mji mkuu wa Nigeria, Abuja kwa lengo la kuhudhuria Kongamano la Usalama la Afrika Magharibi.
Hii ni mara ya tatu kwa Hollande kuitemebelea Jamhuri ya Afrika ya Kati baada ya kuitembelea nchi hiyo Desemba mwaka 2013 na Februari mwaka 2014. Akiwa mjini Bangui, Hollande ametembelea mtaa wa Waislamu kama njia ya kuonyesho kuwa vita vya ndani nchini humo vimemalizika. Itakumbukwa kuwa katika kilele cha vita vya ndani CAR, mitaa yenye Waislamu wengi ilihujumiwa vikali na genge la Wakristo wajulikanao kama Anti-Balaka ambapo Waislamu waliuawa kwa umati huku waliosalia wakiutoroka mji huo. Hivi sasa usalama umerejea kwa kiasi fulani CAR na Waislamu wameanza kurejea katika nyumba zao.
Weledi wa mambo wanaamni kuwa, lengo la Hollande kuitembelea tena CAR, hasa wakati huu ukiwa umesalia mwaka mmoja kabla kumalizika kipindi cha urais wake ni jambo linaloashiria kuwa anataka kutumia suala la kumalizika mgogoro CAR katika kampeni zake za uchaguzi. Aidha lengo jingine la safari ya Hollande huko CAR ni kutangaza kumalizika oparesheni za askari wa Ufaransa huko CAR ifikapo Desemba mwaka huu.
Wakati mgogoro wa CAR ulipoanza Desemba mwaka 2013 ambapo kulijiri mapigano makali baina ya vikosi vya Seleka na waasi wa Anti-Balaka, takribani wanajeshi 2,000 wa Ufaransa, maarufu kama Sangaris, walielekea katika nchi hiyo ya kati mwa Afrika kwa kisingizio cha kulinda amani. Hivi sasa ni askari 650 wa Ufaransa ndio waliobakia CAR. Imedokezwa kuwa askari 100-200 wa Ufaransa watasalia katika nchi hiyo.
Inaoneka safari ya rais huyo huko CAR pia ina ujumbe mwingine ambao ni kuwa, Hollande anataka kuthibitisha tena kuwa Ufaransa ingali na ushawishi mkubwa barani Afrika. Aidha Hollande anataka kusafisha sura iliyochafuka ya Ufaransa kama mkoloni wa zamani barani Afrika na kuarifisha nchi yake kama mshirika wa kuaminika.
Ni kwa msingi huo ndio katika safari yake CAR Hollande ameahidi kusaidia ujenzi mpya wa nchi hiyo katika sekta kama vile za afya, miundomsingi na elimu. Aidha Ufaransa imebaini kuwa iko tayari kutuma vikosi vyake Afrika iwapo kutakuwepo sababu maalumu.
Imearifiwa kuwa askari wa Ufaransa walioko CAR watajiunga na Kikosi cha Umoja wa Mataifa nchini humo MINUSCA na kushirikiana pia na kikosi cha Umoja wa Ulaya kinachotoa mafunzo kwa wanajeshi wa nchi hiyo.
Hollande anajaribu kupandisha hadhi ya Ufaransa Afrika katika hali ambayo askari wa Ufaransa huko CAR wamehusishwa na kashfa kadhaa za udhalilishaji kijinsia. Umoja wa Mataifa uliwahi kutoa taarifa iliyowahusisha askari 14 wa Ufaransa waliokuwa CAR waliowabaka watoto wadogo na kuwadhalilisha kijinsia.
Kufuatia tuhuma hizo, jeshi la Ufaransa ambalo limezoea kuingilia mambo ya ndani Afrika sasa linakabiliwa na kashfa inayotokana na sera za kujipenyeza Afrika.
chanzo;parstoday.

Comments