Mgombea urais wa wapinzani Kongo aitwa mahakamani.

Mwendesha mashtaka mkuu wa mji wa Lubumbashi, kusini mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo amemwita mahakamani mgombea wa urais wa muungano wa wapinzani.
Shirika la habari la Xinhua limesema kuwa, jana mwendesha mashtaka mkuu wa Lubumbashi alimwita mahakamani Moise Katumbi, mgombea urais wa muungano wa upinzani kwa tuhuma za kuajiri mamluki kadhaa wa Kimarekani. Hata hivyo Moise Katumbi amekanusha tuhuma hizo.
Moise Katumbi, milionea ambaye aliwahi kuwa gavana wa Katanga na mpinzani mkubwa wa Rais Joseph Kabila wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo anadai kuwa hajapokea barua yoyote ya kumtaka afike mahakamani.
Kabla ya hapo Waziri wa Mahakama wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, Alexis Thambwe Mwamba, alikuwa ametoa amri kwa mwendesha mashtaka mkuu kuchunguza madai kuwa Moise Katumbi aliajiri mamluki kadhaa wa Kimarekani.
Katika upande mwingine, Ubalozi wa Marekani mjini Kinshasa umeonesha uungaji mkono wake kwa mtuhumiwa huyo ukidai kuwa, madai hayo si kweli.
Habari nyingine zinasema kuwa, Katumbi amewaandikia barua askari wa kulinda amani wa Umoja wa Mataifa akiwaomba wamlinde.
chanzo;parstoday

Comments