Madaktari wasio na mpaka wakosoa uamuzi wa Kenya wa kutaka kufunga kambi za wakimbizi.

Shirika la Madaktari Wasio na Mipaka (MSF) limekosoa uamuzi wa serikali ya Kenya wa kutaka kufunga kambi ya wakimbizi za Dadaab na Kakuma.
Shirika hilo limeonya katika taarifa yake kwamba, kutekelezwa uamuzi huo wa serikali ya Kenya kutapelekea maelfu ya wakimbizi kukabiliwa na hali mbaya.
Shirika la Madaktari Wasio na Mipaka (MSF) limeitaka serikali ya Kenya kufikiria upya uamuzi wake wa kutaka kuzifunga kambi za wakimbizi za Dadaab na Kakuma.
Aidha shirika hilo limeyataka mashirika na taasisi za utoaji misaada zilizoko Kenya kuendelea na shughuli zao za ugawaji misaada klwa wakimbizi walioko katika kambi hizo.
Siku chache zilizopita Kenya ilitangaza kuwa, inatathmini suala la kufunga hivi karibuni kambi zote za wakimbizi nchini humo zikiwemo za Dadaab na Kakuma zenye idadi kubwa ya raia wa Somalia.
Katibu Mkuu wa Wizara ya Masuala ya Ndani Karanja Kibicho alinukuliwa na vyombo vya habari akisema kuwa, serikali ya Nairobi imechukua uamuzi huo kutokana na changamoto za kiuchumi na kiusalama na haswa mashambulizi ya kigaidi ya mara kwa mara.
Katika kufanikisha mpango huo wa kufunga kambi hizo, Wizara ya Mambo ya Ndani ya Kenya imefutilia mbali Idara ya Masuala ya Wakimbizi huku ikiitaka jamii ya kimataifa kuisaidia katika kufanikisha azma yake hiyo.
Kenya ni mwenyeji wa wakimbizi zaidi ya laki 6 haswa katika kambi za Dadaab na Kakuma ambao wamekuwa nchini kwa takriban robo karne.
chanzo;parstoday.

Comments