‘Liwale haina kituo cha Polisi’.

LIWALE ni miongoni mwa wilaya 65 nchini ambazo hazijajengewa vituo vya Polisi, imefahamika. Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Hamad Yussuf Masauni alibainisha hilo jana bungeni wakati akijibu swali la Mbunge wa Liwale, Zuberi Kuchauka (CUF).
Naibu Waziri alisema si kweli kwamba wilaya ya Liwale ndiyo wilaya pekee nchini kutokuwa na Kituo cha Polisi na nyumba za watumishi. “Hata hivyo, serikali inajitahidi kujenga vituo vya Polisi kwa awamu kwa kadri hali ya kibajeti inavyoruhusu,” alisema Naibu Waziri.
Katika swali lake, Kuchauka alihoji serikali ina mpango gani wa kujenga jengo la Kituo cha Polisi Wilaya ya Liwale sambamba na nyumba za watumishi, na lini Tarafa ya Kibutuka itapata kituo kidogo cha Polisi ili kulinda wafanyabiashara wa mazao ya ufuta wanaofika katika tarafa hiyo.
Naibu Waziri alisema ili kusogeza huduma ya Polisi kwa wananchi, ni azma ya serikali kujenga kituo cha Polisi kila tarafa na kupeleka wakaguzi wa Polisi kuongoza vituo hivi. “Hata hivyo, kuna kata nne (Kibutuka, Mirui, Kiangala na Nangano) za Tarafa ya Kibutuka kuna askari kata wanaotoa huduma kwa wananchi,” alisema Naibu Waziri.
Aidha, alisema katika kutekeleza azma hiyo, tayari Jeshi la Polisi limeshapeleka wakaguzi katika baadhi ya tarafa. Akijibu swali la nyongeza la Kuchauka kuhusu lini ujenzi wa kituo cha Polisi Liwale utaanza, Naibu Waziri alisema fedha zitakapopatikana, Liwale itapewa kipaumbele.
chanzo;habarileo.

Comments