Kukombolewa na jeshi la Nigeria wasichana mia moja wa shule waliokuwa wakishikiliwa mateka na Boko Haram.
Jeshi la Nigeria limefanikiwa kuwakomboa mabinti 100 wanafunzi waliokuwa wakishikiliwa mateka na kundi la kigaidi la Boko Haram.
Sani Usman msemaji wa jeshi la Nigeria ametangaza kuwa, katika operesheni hiyo ya kuwakomboa wasichana hao wa shule katika jimbo la Borno, wanachama 35 wa kundi hilo la Boko Haram wameuawa.
Maafisa wa kijeshi wa Nigeria wamesisitiza kuwa, wasichana wengine waliobakia ambao wanaendelea kushikiliwa mateka na wanamgambo wa Boko Haram nao watakombolewa muda sio mrefu.
Ikumbukwe kuwa, wasichana wapatao 267 walitekwa nyara na kundi la Boko Haram Aprili mwaka 2014 ambapo 75 kati yao walifanikiwa kutoroka. Wasichana hao wa shule ya bweni ya Chibok akthari yao ni Wakristo.
Kwa mara ya mwisho wasichana hao walishuhudiwa katika mkanda mmoja wa video uliosambazwa na Boko Haram Mei mwaka 2014.
Hivi Karibuni jeshi la Nigeria lilitangaza pia kukombolewa wasichana kadhaa kutoka mikononi mwa wanamgambo wa Boko Haram ambao wametenda jinai kubwa nchini Nigeria na katika nchi za jirani.
Katika siku za hivi karibuni jeshi la Nigeria likishirikiana na lile la Cameroon limepata mafanikio makubwa katika operesheni zao dhidi ya wanamgambo wa Boko Haram.
Muungano huo wa kijeshi Jumapili iliyopita ulifanikiwa kuteketeza kambi tatu za wanamgambo hao zilizokuwa zikitumika kutoa mafunzo.
Aidha katika operesheni hiyo ya kijeshi makumi ya wanachama wa Boko Haram wameuawa huku watu 52 waliokuwa wakishikiliwa mateka na wanamgambo hao wakikombolewa.
Inavyoonekana ni kuwa, serikali ya Rais Muhammadu Buhari imelipa kipaumbele suala la kupambana na kundi la kigaidi la Boko Haram.
Jumamosi iliyopita, Abuja mji mkuu wa Nigeri ulikuwa mwenyeji wa mkutano wa viongozi wa nchi kadhaa za Kiafrika, Rais wa Ufaransa na maafisa wa Umoja wa Ulaya na Marekani ambapo suala la uratibu wa kukabiliana na wanamgambo wa Boko Haram lilijadiliwa kwa kina.
Wachambuzi wa mambo wanaamini kwamba, ushindi wa hivi karibuni dhidi ya Boko Haram umeboresha nafasi ya Rais Muhammad Buhari. Kabla ya hapo Rais Buhari alikuwa akiandamwa na kukosolewa na wapinzani kutokana na kuongezeka mashambulio ya kigaidi nchini humo.
Mashambulio ya kigaidi nchini Nigeria Februari mwaka huu yalipelekea kusimamishwa uchimbaji mafuta.
Baadhi ya wajuzi wa mambo wanaona kuwa, kubadilishwa siasa za serikali tangu
kuingia madarakani Rais Muhammadu Buhari na kuanza tena machafuko hakujatokea sadfa na hivi hivi tu.
Waasi wanamtuhumu Rais Buhari kwamba, amekuwa akilipa umuhimu suala la kuchunga vyanzo vya mafuta nchini humo kuliko roho za watu.
chanzo;parstoday.
Comments