Kiongozi wa upinzani nchini Uganda akamatwa kwa tuhuma za uhaini.

Kizza Besigye, Kiongozi wa chama cha upinzani nchini Uganda cha Forum for Democratic Change, anazuiliwa jela kwa tuhuma za kufanya uhaini dhidi ya nchi hiyo. Kesi yake imepangwa kusikilizwa mwanzoni mwa mwezi ujao wa Juni.
Siku moja kabla ya kuapishwa rasmi Rais Yoweri Museveni ili ahudumie kipindi kingine cha urais wa nchi hiyo, Kizza Besigye alidhihiri ghafla kwenye mkusanyiko wa wafuasi wake ambao walimuapisha kuwa rais wa Uganda, jambo ambalo limechukuliwa na serikali ya Kampala kuwa usaliti kwa nchi hiyo.
Awali polisi ya Uganda ilikuwa imemtuhumu Besigye kwa kuzua vurugu katika mji mkuu Kampala na kuhatarisha usalama wa taifa. Mvutano wa kisiasa umefikia kilele kufuatia malumbano yaliyozuka kati ya serikali na wapinzani baada ya kufanyika uchaguzi mkuu uliojaa utata hapo tarehe 18 Februari. Kizza Besigye, ambaye alikuwa mpinzani mkuu wa Rais Yoweri Museveni katika uchaguzi amekataa kukubali rasmi matokeo ya uchaguzi huo akisema kuwa uchakachuaji mkubwa ulifanywa na vibaraka na waungaji mkono wa serikali ya Kampala ili kumyima ushindi wa wazi. 
Tokea wakati huo wapinzani wamekuwa wakifanya maandamano ya amani kulalamikia maotokeo hayo na kutaka kura zihesabiwe upya.
Hii si mara ya kwanza kwa Museveni kutuhumiwa kufanya udanganyifu katika uchaguzi wa nchi hiyo. Kiongozi huyo ambaye aliingia madarakani mwaka 1986, amekuwa akiongoza nchi hiyo kwa mkono wa chuma kupitia chama tawala cha National Resistance Movement NRM. 
Kama walivyofanya viongozi wengine wakongwe wa Afrika, Museveni aliongoza Uganda kwa muda mrefu kupitia mfumo wa chama kimoja lakini hatimaye alisalimu amri mbele ya mashinikizo ya kisiasa ya ndani na nje na kukubali nchi hiyo itawaliwe na mfumo wa vyama vingi, mfumo ambao ulipitishwa kufutia mabadiliko ya katiba yaliyofanyika mwaka 2005 kupitia kura ya maoni.
Pamoja na hayo Museveni alifanya ujanja wa kuwasilisha bungeni marekebisho ya katiba ili kuondoa kipengee kilichomzuia kugombea tena urais wa nchi hiyo na hivyo kujiandalia nafasi ya kuendelea kutawala. Hatua hiyo iliwakasirisha sana wapinzani. Mbali na malalamiko ya kisiasa, ughali wa maisha na mdororo wa uchumi ni changamoto kubwa zinazoikabili serikali ya Museveni kwa hivi sasa. 
Wapinzani wanasema licha ya Museveni kutumia vibaya mali ya umma, udhibiti wake juu ya vyombo na taasisi tofauti za serikali ndio uliompa ushindi katika uchaguzi wa hivi karibuni. Wapinzani wa kisiasa wa Museveni wanamtuhumu kuwa badala ya kuhudumia nchi amekuwa aking'ang'ania madaraka kwa lengo la kudhamini maslahi ya nchi za Magharibi. 
Licha ya baadhi ya wajuzi wa mambo kusema kuwa malalamiko na maandamano ya hivi karibuni ya wapinzani yanatia wasiwasi, lakini kuna wengine wanaosema kuwa Uganda bila ya Museveni ni jambo lisilowezekana.
chanzo;parstoday.

Comments