Kikao cha kuzuia mgomo wa nchi nzima Nigeria chavunjika.


Kikao kilichokuwa kimeitishwa na serikali ya Nigeria kwa ajili ya kujaribu kuzuia kufanyika mgomo wa nchi nzima katika nchi hiyo ya magharibi mwa Afrika kilivunjika jana usiku bila kufikiwa natija yoyote. Nyogeza ya asilimia 67 ya mafuta kwa mara nyingine tena imeongeza malalamiko ya wananchi wa nchi hiyo.
Chama cha wafanyakazi wa Nigeria cha Nigeria Labour Congress NLC kimesema kuwa maafisa wake walilazimika kuondoka kwenye kikao hicho kutokana na kuwa wawakilishi wa serikali kuu ya Nigeria hawakuwa hata tayari kusikiliza mapendekezo ya kutazamwa upya nyongeza hiyo ya mafuta na nyingine iliyokuwa imeongezwa awali kwenye matumizi ya umeme. 
Chama hicho na vingine vilivyo chini yake kikiwemo cha Trade Union Congress, TUC pamoja na jumuiya za kiraia vimetaka mgomo wa wote ufanyike nchini humo hadi pale serikali itakapotekeleza matakwa yao ya kupunguza bei ya mafuta nchini. 
Katika hali ya hivi sasa mbali na changamoto za usalama zinazosababishwa na ugaidi wa Boko Haram, hali mbaya ya uchumi na ughali wa maisha unaoendelea kuongezeka kila siku ni matatizo makubwa yanayoikabili serikali ya Abuja. 
Serikali hiyo inahitajia pesa na misaada ya kiuchumi kuliko wakati mwingine wowote. Asilimia 70 ya pato la Nigeria linatokana na uuzaji nje mafuta ghafi ambayo bei yake imepungua sana katika masoko ya kimataifa. 
Tatizo jingine ni kuwa uchimbaji mafuta wa nchi hiyo umepungua sana na kufikia kiwango cha chini zaidi tokea mwaka 1994. 
Kuongezeka ghasia katika eneo la uchimbaji mafuta la Niger Delta ni miongoni mwa matatizo yanayoikabili serikali ya Nigeria. 
Kwa mujibu wa ripoti, uzalishaji mafuta wa Nigeria umepungua kutoka mapipa milioni 2.2 na kufikia milioni 1.4 kwa sasa. 
Awali Waziri wa Mafuta wa Nigeria alikuwa ameelezea wasiwasi wake kuhusiana na athari mbaya ya machafuko hayo kwa uzalishaji mafuta na uchumi wa nchi hiyo. 
Kuongezeka ghasia katika eneo hilo na vilevile kutonunuliwa vifaa na mitambo mipya katika sekta ya mafuta ya Nigeria ni mambo mawili yanayoathiri pakubwa azalishaji mafuta wa nchi hiyo. 
Machafuko yanayoendelea huko Niger Delta yameongeza mashinikizo dhidi ya serikali ya Abuja. Wapinzani wanaitaka serikali kuchukua hatua za haraka na sahihi katika kumaliza uasi na machafuko katika eneo hilo. 
Katika miaka kadhaa iliyopita machafuko na utekaji nyara katika sekta ya mafuta katika eneo hilo ulikuwa umepungua kutokana na msamaha uliotolewa na serikali mwaka 2009 kwa wanamgambo wanaobeba silaha wa eneo hilo. 
Katika kipindi cha utekelezaji wa msamaha huo, viongozi wa zamani wa wanamgambo walipata faida kubwa kifedha kutokana na mikataba ya kulinda mabomba ya mafuta waliyotia saini na serikali ya rais wa wakati huo wa Nigeria Goodluck Jonathan, na wakati huohuo wakawa wanauza mafuta kwa njia za magendo. 
Lakini eneo la Niger Delta limekuwa likishuhudia machafuko tokea wakati wa kuingia madarakani Rais Muhammadu Buhari. 
Buhari ametangaza kuwa ameazimia kukabiliana vilivyo na bila kulegeza msimamo na makundi ya wanagambo wa Nigera Delta ambao wanaharibu mabomba na taasisi za mafuta katika eneo hilo ambalo ndilo linalozalisha mafuta mengi zaidi nchini humo. 
Amelitaka jeshi la wanamaji wa nchi hiyo kujitayarisha kutekeleza operesheni za kijeshi dhidi ya kundi la waasi wa eneo hilo. 
Pamoja na hayo lakini uzoefu unaonyesha kuwa juhudi za serikali za kupambana na wizi pamoja na uharibifu wa mabomba ya mafuta ghafi katika eneo la Niger Delta hazijakuwa na natija ya kuridhisha.
chanzo;parstoday.

Comments