Karibu katika kuangalia kumbu kumbu ya siku zilizo pita inayofanana na siku kama ya leo.

Jumamosi, 14 Mei 2016

Leo ni Jumamosi tarehe 7 Shaaban mwaka 1437 Hijria, sawa na tarehe 14 Mei mwaka 2016 Miladia.

Siku kama ya leo miaka 441 iliyopita, ardhi ya Angola ilikaliwa kwa mabavu na mkoloni Mreno. Kabla ya Wareno kuwasili Angola, ardhi hiyo ilikuwa sehemu ya utawala wa Kiafrika wa Guinea. Baada ya Wareno kuidhibiti nchi hiyo walianzisha vituo vya biashara katika maeneo yake yote ya pwani. Baada ya kumalizika vita vya Pili vya Dunia, harakati kadhaa zilianzishwa nchini Angola kwa lengo la kuipatia uhuru nchi hiyo. Hatimaye mwaka 1975 harakati za wapigania uhuru zilizaa matunda baada ya nchi yao kupata uhuru.

Katika siku kama ya leo miaka 205 iliyopita, nchi ya Paraguay ilipata uhuru. Paraguay iligunduliwa katika karne ya 16 Miladia na Muhispania mmoja na ikawa chini ya utawala wa Uhispania kwa zaidi ya karne mbili. Baada ya uhuru nchi hiyo ilitawaliwa na serikali ya kidikteta na kulishudiwa majaribio kadhaa ya mapinduzi na kila aliyekuja madarakani aliongoza kidikteta. Uchaguzi wa kwanza huru wa Rais ulifanyika nchini humo mwaka 1989. Kijiografia Jamhuri ya Paraguay inapatikana huko Amerika Kusini baina ya nchi za Brazil, Argentina na Bolivia. 

Miaka 61 iliyopita katika siku kama ya leo mkataba wa kisiasa na kijeshi ulitiwa saini baina ya nchi nane za kikomonisti barani Ulaya. Makubaliano hayo yaliyojulikana kama The Warsaw Pact yalitiwa saini katika mji mkuu wa Poland, Warsaw na lengo lake lilikuwa ni kukabiliana na Mkataba wa Shirika la Kujihami la Nchi za Magharibi (NATO) uliotiwa saini na madola ya magharibi waitifaki wa Marekani. Nchi zilizotia saini makubaliano hayo ziliahidi kutotumia nguvu na mabavu katika ushirikiano wao. Aidha zilikubaliana kwamba, kushambuliwa kijeshi mwanachama mmoja ni sawa na kuchokozwa nchi zote wanachama. Hatimaye baada ya miaka 36, mkataba huo ulifutwa mwaka 1991 baada ya nchi hizo kukutana huko Budapest mji mkuu wa Hungary. 

Na katika siku kama ya leo miaka 68 iliyopita, utawala bandia wa Israel ulitangaza uwepo wake baada ya kufanya mauaji makubwa ya umati dhidi ya Wapalestina.  Askari wa Uingereza waliikalia kwa mabavu Palestina kufuatia kushindwa utawala wa Othmania wakati wa Vita Vikuu vya Kwanza vya Dunia. Miaka mitano baadaye Jumuiya ya Kimataifa ikaibidhi Palestina kwa Uingereza na kuifanya chini ya mamlaka ya mkoloni huyo. Novemba mwaka 1947 Umoja wa Mataifa ukapasisha azimio lililotaka kuundwa madola mawili ya Kiarabu na Kiyahudi huko Palestina. 
chanzo;parstoday

Comments