Kikao cha pamoja cha Italia na Afrika kilianza siku ya Jumatano Mei 18 huko Rome, mji mkuu wa Italia kwa lengo la kuchunguza hujuma ya wahamiaji na wahajiri haramu wa Kiafrika kuelekea nchi za Ulaya na vilevile kujadili njia za kuisaidia serikali ya umoja wa kitaifa nchini Libya irudishe uthabiti nchini.
Rais Idriss Deby wa Chad ambaye nchi yake kwa sasa ndio mwenyekiti wa Umoja wa Afrika amesema kuwa umoja huo unaiunga mkono serikali ya umoja wa kitaifa ya Libya katika kila upande.
Akizungumza katika kikao hicho, Paolo Gentiloni Silveri Waziri wa Mambo ya Nje wa Italia amesema kuwa nchi zote wanachama wa Umoja wa Ulaya zina hamu ya kuona serikali ya umoja wa kitaifa ya Libya inayoongozwa na Fayez al-Sarraj ikirejesha utulivu na kueneza mamlaka yake katika pembe zote za nchi hiyo.
Kwa upande wake Musa Faki Mohammed, Waziri wa Mambo ya Nje wa Libya amesema katika kikao hicho kwamba machafuko na ghasia katika nchi hiyo ya Kiafrika zimeifanya nchi hiyo ya kaskazini mwa Afrika kuwa maficho kwa magaidi.
Kwa mtazamo wa waziri huyo, wahajiri haramu kutoka nchi za Kiafrika ambao wana nia ya kuelekea Ulaya kwa ajili ya kupata kazi na maisha bora wanaichagua Libya kuwa njia bora zaidi ya kufika katika nchi za Ulaya.
Kwa msingi huo, Waziri wa Mambo ya Nje wa Libya amezishukuru nchi 25 za Umoja wa Ulaya ambazo wiki iliyopita zilichukua uamuzi wa kuiondolea nchi hiyo ya Kiafrika vikwazo vya silaha.
Waziri huyo amezitaka pande zote hasimu nchini Libya zishirikiane, kufuata njia ya amani na maelewano ya kitaifa na kuikubali serikali ya umoja wa kitaifa ya nchi hiyo. Waziri wa Mambo ya Nje wa Italia aliwaambia mawaziri wenzake wapatao 40 kutoka nchi za Kiafrika kwamba iwapo nchi za Kiafrika zitasaidia katika kuwarejeshwa makwao wahamiaji haramu ambao hivi sasa wako katika nchi za Ulaya, basi Umoja wa Ulaya utazidisha msaada wake wa kifedha na kuwekeza zaidi barani Afrika.
Mwaka uliopita viongozi wa Umoja wa Ulaya waliafiki kuzipa nchi za Afrika msaada wa Euro bilioni moja na milioni 800.
Pamoja na hayo lakini mashirika ya misaada ya kibinadamu na serikali za Kiafrika zinasema jambo muhimu ni kuimarishwa ushirikiano wa jamii ya kimataifa na hasa wa nchi za Ulaya katika kutatua matatizo yanayosabisha uhamiaji kama vile umasikini na ukosefu wa ajira barani Afrika.
Italia ambayo inapakana na bahari ya Mediterranean ndicho kituo cha kwanza barani Ulaya kinachotumiwa na wahamiaji haramu wa Kiafrika wanaoelekea Ulaya wakiwa na matumaini ya kupata kazi na maisha bora.
Kuendelea kwa vita vya ndani huko Syria na mgogoro wa Iraq ni mambo mengine ambayo yameongeza idadi ya wahamiaji na wakimbizi wanaoingia barani Ulaya na hivyo kuzisababishia nchi za bara hizo matatizo mengi.
Kwa mujibu wa takwimu, kati ya mwaka 2010 na 2015 wahajiri wa Kiafrika wapatao milioni mbili walifika katika bandari za Italia.
Kwa kutoa ahadi ya kuzidishwa misaada ya kifedha na uwekezaji wa kigeni barani Afrika, Waziri wa Mambo ya Nje wa Italia amejaribu kuwashawishi viongozi wa Kiafrika wajaribu kudhibiti mipaka yao na kuwazuia wahamiaji haramu wanaoelekea barani Ulaya.
Wakati huohuo Mankeur Ndiaye, Waziri wa Mambo ya Nje wa Senegal ameonya kuwa Umoja wa ulaya hautafanikiwa kirahisi kufunga mipaka yake mbele ya hujuma ya wahamiaji wa Kiafrika.
Amesema, hii ni kwa sababu nchi za Ulaya zitapata hasara kubwa iwapo zitachukua hatua ya kuwazuia wahajri wa Afrika kuingia barani Ulaya kutokana na bara hilo kutegemea pakubwa kiuchumi nguvu kazi ya Waafrika.
Waziri huyo alikuwa akiashiria mamilioni ya Waafrika ambao kwa miaka mingi wamekuwa wakiishi na kufanya kazi katika mazingira magumu na kwa mishahara ya chini katika nchi za Ulaya na hivyo kuchangia pakubwa katika ujenzi na ustawi wa uchumi wa bara hilo. sehemu kubwa ya wahamiaji haramu wanaoelekea barani Afrika ni vijana.
Kizazi cha vijana ambacho kinakabiliwa na uhaba wa ajira, umasikini na machafuko katika nchi zao zikiwemo za Libya na Niger ndicho kinachoamua kuhama nchi zao na kuelekea Ulaya kwa lengo la kutafuta kazi na maisha bora.
Ni kwa msingi huo ndipo Waziri wa Mambo ya Nje wa Senegal akaamini kwamba katika kukabiliana na wimbi la wahamiaji wanaoelekea Ulaya, mazingira yanayofaa yanapaswa kutayarishwa kwa madhumuni ya kuwaandalia vijana wa Kiafrika nafasi za kazi na vyanzo vipya vya pato la kuendeshea maisha.
chanzo;parstoday.
Comments